HAKIKISHENI WATOTO WOTE WALIOCHAGULIWA WANARIPOTI SHULENI -MSIGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, January 15, 2023

HAKIKISHENI WATOTO WOTE WALIOCHAGULIWA WANARIPOTI SHULENI -MSIGWA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Sita katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Januari 15, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Sita katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Januari 15, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma.

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kwenda kujiunga na elimu ya sekondari wanaripoti shuleni.

Msigwa ameyasema hayo leo Januari 15,2023 katika kikao na waandishi wa habari ambapo amesema serikali inagharamia elimu ya msingi na sekondari kwa kutoa shilingi Bilioni 29.8 kila mwezi na pia imetoa maelekezo mahususi juu ya michango kwa wanafunzi wanaoripoti shuleni, lengo likiwa ni vikwazo vinavyoweza kusababisha wanafunzi kutoripoti shuleni.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jiji la Dodoma ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kubadili taswira ya Mkoa huo na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Aidha ameongeza kuwa kwenye elimu pamoja na mambo mengine serikali imeleta shilingi Bilioni 6.8 ambazo zimejenga madarasa 339 ambayo yameanza kutumiwa na wanafunzi wa Kidato cha kwanza mwaka mwaka huu.

“Madarasa haya pamoja na yaliyokuwepo yamewezesha wanafunzi wote walioachaguliwa kuanza kidato cha kwanza kuanza kwa mara moja badala ya kuanza kwa mafungu mafungu,”amesema Msigwa.

Amesema mwaka huu 2023 Watoto walioandikishwa kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza ni 1,446,067 wakiwemo wenye mahitaji maalum 2,942, hiyo ikiwa ni sawa na 88.48% ya wanafunzi 1,634,365 wanaotarajiwa kuandikishwa na kazi ya uandikishaji ikiendelea.

Kwa upande wa sekondari wanafunzi walioripoti kuanza kidato cha kwanza 354,277 wakiwemo wenye mahitaji maalum 697, wanafunzi ikiwa ni sawa na 33% ya matarajio ya kupokea wanafunzi 1,070,941 waliochaguliwa kujiunga Kidato cha kwanza.

“Lakini pia tumeandikisha wanafunzi 14,581 wa MEMKWA (Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa), kati yake 334 ni wenye mahitaji maalum, tumeandikisha pia wanafunzi wa awali 1,129,324 wakiwemo 2,371 wenye mahitaji maalum,”amesema Msigwa.

No comments:

Post a Comment