KUTOZINGATIA MWONGOZO WA UANDAAJI WA MIKATABA YA HUDUMA KWA MTEJA KATIKA UTUMISHI WA UMMA INASABABISHA WATUMISHI KUENDELEA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA-MHAGAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 31, 2023

KUTOZINGATIA MWONGOZO WA UANDAAJI WA MIKATABA YA HUDUMA KWA MTEJA KATIKA UTUMISHI WA UMMA INASABABISHA WATUMISHI KUENDELEA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA-MHAGAMA


Na Okuly Julius-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Jenista Mhagama, amesema Ofisi hiyo imebaini uwepo wa  baadhi ya Taasisi za Umma ambazo hazina Mkataba wa Huduma kwa Mteja, na zingine mikataba yao imeshapitwa na wakati au kuandaliwa bila kuzingatia Mwongozo wa Serikali wa kuandaa Mikataba.

Mhagama ameyasema hayo leo Januari 31,2023 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika utumishi wa Umma.

Waziri huyo amesema kuwa Taasisi hizo kwa kutozingatia Mwongozo wa uandaaji wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja imepelekea Taasisi kuwa na Mikataba isiyokidhi viwango vya huduma vinavyotakiwa kutolewa, na hii ni kutokana na kukosekana kwa utayari wa Viongozi wa Taasisi za Umma kubadilisha mitizamo ya kiutendaji, kukubali mabadiliko na kuendelea kufanya kazi kwa mazoea kwenye Taasisi zao.


"Ofisi imebaini baadhi ya Taasisi za Umma hazifanyi ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora hali inayosababisha Taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa mazoea bila matokeo tarajiwa,"

Na kuongeza kuwa "Ofisi pia imebaini baadhi ya Taasisi kuandaa/kuhuisha mikataba ya Huduma kwa Mteja bila kushirikisha Wataalam husika na kupata idhini ya matumizi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,"amesema Mhagama

Mhagama ameongeza kuwa ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha Taasisi zote za Umma ya kuwa na huduma bora zinazotolewa kwa Wananchi wote wa Tanzania na wageni, kupitia Mikataba ya Huduma kwa Mteja,amezielekeza Taasisi zote za Umma (Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ,kuandaa/kuhuisha na kuwasilisha katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mikataba iliyoandaliwa au kuhuishwa kwa ajili ya kupata idhini ya matumizi.


" Ili kuhakikisha maelekezo haya ya Serikali yanatekelezwa na wananchi wanahabarishwa viwango vya utoaji wa huduma ndani ya Serikali kupitia Taasisi za Umma, Mikataba itakayowasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kukidhi viwango itazinduliwa kwa pamoja katika uzinduzi utakaofanyika katika awamu mbili,"

"Uzinduzi wa Awamu ya Kwanza utahusisha Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, utafanyika tarehe 28 Februari 2023,Uzinduzi wa Awamu ya Pili utahusisha Wakala za Serikali, Idara zinazojitegemea na Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali utafanyika tarehe 28 Aprili 2023,"


Ambapo kila Taasisi zilizopo katika makundi hayo zinatakiwa kuwasilisha nakala za Mikataba hiyo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wiki mbili kabla ya tarehe ya uzinduzi.

Mkataba huo unamuwezesha Mwananchi kufahamu huduma zinazotolewa na Taasisi ya Umma, Viwango vya utoaji wa huduma, Wajibu wa Taasisi kwa mpokea huduma, Wajibu na haki ya mteja au mpokea huduma, Njia zitakazomuwezesha mteja kupokea na kutoa mrejesho wa huduma zilizotolewa na njia za Mawasiliano na taasisi.

No comments:

Post a Comment