SERIKALI YATOA MWONGOZO KWA TAASISI ZAKE KUHAMIA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, January 16, 2023

SERIKALI YATOA MWONGOZO KWA TAASISI ZAKE KUHAMIA DODOMA


Na Okuly Julius-Dodoma 

SERIKALI imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma kwa awamu.

Kufuatia muongozo huo imezielekeza taasisi 42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha.

Akizungumza Jijini Leo Januari16,2023, wakati akikabidhi vibali vya ujenzi wa Ofisi za taasisi Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene alisema taasisi nyingine 36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha.

Katika hatua nyingine Simbachawene amesema taasisi 19 zitahamia katika mwaka fedha 2024/25 wakati taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.

"Serikali ilikuwa na jumla ya taasisi 189 zilizokuwa zinatekeleza majukumu yake Jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, kutokana na zoezi la Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma, taasisi 55 za serikali zimetekeleza maelekezo hayo kwa kuamua kujenga ofisi zake Dodoma,"alisema

Ameongeza kuwa "Hadi sasa taasisi 20 zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na hatua mbalimbali za ujenzi, taasisi nyingine 19 zipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi baada ya kupata vibali vya ujenzi kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Simbachawene amebainisha kuwa majengo ya taasisi za serikali yanajengwa katika maeneo ya NCC Link, Medeli, Njedengwa Mtumba na Kikombo kwa kufuata mwongozo uliopo katika Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma.

Amesema ujenzi unaoendelea unategemewa kubadili mandhari ya Jiji la Dodoma pamoja na kupunguza changamoto ya ofisi na hivyo kuwezesha zoezi la serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma kwa ufanisi zaidi.

Kwa mujibu wa Simbachawene alisema serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi 26 za wizara yanayojengwa katika awamu ya pili.

Amefafanua kuwa ujenzi huo umefikia wastani wa takriban asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba mwaka huu kwa gharama ya sh. bilioni 675.

"Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi za uboreshaji wa miundombinu ya miradi ya kimkakati Dodoma ikiwemo ujenzi wa uwanja Ndege Msalato utakaogharimu sh. billioni 165 ambao ujenzi wake umefikia asiimia 11, ujenzi wa barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 112 na utagharimu sh. bilioni 221 ambao ujenzi umefikia asilimia 20, ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambalo litazalisha maji mita za ujazo 130,000 kwa siku na kugharimu sh. bilioni 325.

Ameongeza kuwa”Serikali inaendelea na ujenzi wa mtandao wa maji kutoka Bwawa la Mtera hadi Dodoma utakaozalisha mita za ujazo 128,000 kwa siku, uboreshaji wa barabara za mtandao wa lami katika Jiji la Dodoma na ujenzi wa reli itakayozunguka Jiji la Dodoma ili kurahisisha huduma za usafirishaji na kupunguza msongamano.

Waziri simbachawene amesema serikali inazitaka taasisi zote zinazoendelea na ujenzi Dodoma zihakikishe ujenzi huo unakamilika kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi ikiwemo ubora, muda, bajeti iliyotengwa na thamani ya fedha ili kuleta tija inayotarajiwa.

Amesema taasisi zote zilizoelekezwa kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba zihakikishe zinatekeleza maagizo hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa utekelezaji wake.

“Ofisi ya Katibu Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Mamlaka husika iendelee kuratibu mpango wa serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii Dodoma,

Na kuongeza kuwa “Taasisi nyingine ambazo bado hazijaanza maandalizi ya ujenzi Dodoma ziwasilishe ofisi ya Waziri Mkuu mahitaji ya viwanja vya ujenzi wa ofisi za Taasisi Dodoma kwa ajili ya uratibu wa pamoja.

Simbachawene amezitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa makao makuu katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma za kijamii .

Amezitaja huduma hizo kuwa ni shule na hospitali zenye hadhi ya kimataifa, hoteli za nyota tano, migahawa ya kisasa, kumbi zenye hadhi ya kimataifa, nyumba za kisasa za makazi, huduma za usafiri wa anga na ardhini, utalii, na maduka makubwa

Amekabidhi vibali vya ujenzi wa ofisi za taasisi 20 za serikali kwa lengo la kutambua mchango wa katika uendelezaji wa makao makuu ya nchi kwa kuanza maandalizi ya ujenzi wa taasisi zao na kutoa vyeti vya pongezi kwa taasisi 35 zilizokamilisha na zinazoendelea na hatua mbalimbali za ujenzi.

No comments:

Post a Comment