SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KATIKA SEKTA YA AFYA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 17, 2023

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KATIKA SEKTA YA AFYA.


Na.Elimu ya Afya kwa Umma,Arusha

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo ikiwemo Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika masuala ya Afya kwani yana mchango Mkubwa kwa jamii.

Hayo yamebainishwa leo Februari 17,2023 Jijini Arusha na John Yuda kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga wakati akifunga kikao kazi cha pamoja kati ya Wadau wa Maendeleo na Serikali kuhusu kuainisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji (Health Promotion priority interventional activities) kwa mwaka 2023/2024.

Yuda amesema Wadau wa Maendeleo wana umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa Afua za Elimu ya Afya hivyo Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Ustawi wa Afya Bora unaendelea kuimarika kwa Watanzania.

“Mambo mengi tumekuwa tukishirikiana na Wadau wa Maendeleo, katika kuhudhuria kikao hiki muhimu sisi kama Serikali tunashukuru sana kwa ujio wenu mmeacha majukumu yenu lakini tumekusanyika kwa pamoja na kikao hiki kitakuwa na matokeo chanya kwa ajili ya kuweka mipango yetu kwa maslahi mapana ya taifa”, amesema Yuda.

Aidha, Yuda amesema Changamoto zilizoibuliwa katika uratibu zigeuzwe kama fursa katika kuhakikisha ushirikiano unaimarika zaidi.

“Changamoto tulizoziibua katika masuala ya Coordination ziwe kama fursa hivyo kupitia kikao hiki tumetambua kila mmoja anapotaka kutekeleza majukumu yake aanzie wapi”,amesema.

Kuhusu kuelekea Wiki ya Elimu ya Afya kwa Umma(Health Promotion Week) itakayokwenda sambamba na Siku ya Afya Duniani April 7, 2023 kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Tumaini Haonga, Yuda ametoa Ombi la Kipekee kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuendelea kutoa ushirikiano kuwezesha siku hiyo muhimu.

“Sasa tunaelekea katika wiki ya Health Promotion ambayo pia itaenda sambamba na siku ya Afya Duniani nina Ombi la Kipekee tuendelee kushirikiana katika wiki hiyo muhimu ni wiki kunakuwa na mambo mbalimbali ni muhimu kukaa na kufanya Review na tusipokaa tukafanya pamoja utekelezaji utakuwa wa kusuasua”amesisitiza.

Awali akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya wawakilishi kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mwakilishi kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID)Lulu Msangi amehimiza yote waliyojadili kupitia kikao hicho yasiishie kwenye maandishi bali utekelezaji zaidi ufanyike hasa katika suala la ushirikiano na Elimu ya Afya Kwa Umma katika afua mbalimbali za Uelimishaji wa Afya.

“Tusiishie kwenye maandishi, twende kwenye utekelezaji, bila Wizara hatuwezi kufanya chochote hata kama tuna mamilioni, tuendelee kufanya kazi kuona kuwa impact (matokeo)katika kuhakikisha magonjwa yanapungua kwa kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi”amesema.

Ikumbukwe kuwa kikao kazi cha pamoja kati ya Wadau wa Maendeleo na Serikali kuhusu kuainisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji (Health Promotion priority interventional activities) kwa mwaka 2023/2024 kilianza tarehe 13 Februari, 2023 na kuhitimishwa leo tarehe 17 Februari, 2023 ambapo wadau kwa pamoja wameazimia kuendelea kushirikiana na Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga,Wizara ya Afya pindi wanapotekeleza miradi ya Afya.

No comments:

Post a Comment