Na Mwandishi wetu Morogoro
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuendeleza na kutunza rasilimali za maji hapa nchini ni jambo la msingi na lenye faida kubwa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo kama moja ya urithi katika jamii.
Amesema hayo katika kikao cha Bodi ya Maji ya Taifa mkoani Morogoro na kusisitiza kwa wajumbe wa bodi hiyo kutumia uzoefu wao katika kutoa majibu ya changamoto zinazohusu maji na sio kuegemea katika mabadiliko ya tabianchi kwa sababu miradi ya maji inategemea uwepo wa vyanzo vya maji muda wote
Mhandisi Luhemeja amesema mabadiliko ya hali ya hewa yatumike kubuni mbinu za kuhakikisha maji yanakuwepo nchini, na kuongeza hivi sasa mpango ni kuwa na gridi ya maji nchini, ambayo itaimarisha huduma ya maji katika maeneo yenye upungufu.
Ameitaka Bodi ya Maji ya Taifa kutembelea wadau na kuona changamoto zao ili kupata majibu, kufanya tathmini na kushauri ipasavyo kwa sababu huduma ya maji maana yake ni kuangalia uhai wa Watanzania.
“Tuwe na miundombinu inayotumia maji vizuri na kwa ufanisi” Mhandisi Luhemeja amesema na kuongeza ni vizuri kufanya jambo ambalo kila mwananchi atapata faraja na kuona manufaa yake na kueleza kuwa mwezi Julai 2022 ilizinduliwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Tatu itakayodumu mwaka 2022 hadi 2026 na inahitaji Dola za Marekani bilioni 6.46.
Pia, amesema Wizara ipo katika maandalizi ya Programu ya Uwekezaji katika Sekta ya Maji ambayo itatekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2030 na itagharimu dola za Marekani bilioni 24.7.
Bodi ya Maji ya Taifa inaongozwa na Mwenyekiti Katibu Mkuu mstaafu Mhandisi Mbogo Futakamba.
Tanzania ina maji yanayoweza kupatikana kila mwaka wastani wa mita za ujazo bilioni 126 ambapo mita za ujazo bilioni 105 ni maji juu ya ardhi na mita bilioni 21 ni chini ya ardhi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009 na Mabadiliko yake ya Mwaka 2022, Bodi ya Maji ya Taifa ni chombo cha ushauri kwa Waziri wa Maji.
No comments:
Post a Comment