MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN TARURA MKOA WA TANGA KAZI INAENDELEA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 25, 2023

MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN TARURA MKOA WA TANGA KAZI INAENDELEA


KATIKA miaka miwili ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya kazi ya kufungua barabara za vijijini na mijini mkoani Tanga.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tanga unahudumia mtandao wa barabara wenye kilomita 7373.69 ambapo barabara za lami ni kilomita 141.834, barabara za changarawe kilomita 1795.509, barabara za udongo kilomita 5436.347, madaraja 100, kalavati 5398, boksi kalavati 496 na Madrifti 306.

Kati ya barabara hizo zenye hali nzuri ni kilomita 2,932 sawa na asilimia 40, hali ya kuridhisha ni kilomita 2,712.55 sawa na asilimia 37 na zilizo katika hali mbaya ni kilomita 1,686.2 sawa na asilimia 23.


Akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga, Mhandisi George Tarimo anasema kabla ya bajeti ya TARURA kuongezeka barabara nyingi katika Mkoa wa Tanga zilikuwa katika hali mbaya, asilimia kubwa zilikuwa hazipitiki.

Anasema kuwa hali hiyo ilitokana na fedha iliyokuwa ikitengwa ya Sh bilioni 12.428 kutoka Mfuko wa Barabara kuwa finyu.

“Fedha hizi ziliweza kufanya matengenezo katika maeneo machache tu hali iliyopelekea maeneo mengi kuwa na changamoto ya usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko na huduma za kijamii.” 

Mhandisi Tarimo anasema pia kasi ya kuongeza mtandao wa lami, barabara za changarawe na ujenzi wa madaraja na vivuko ilikuwa ni ndogo kutokana na ufinyu wa bajeti.


Mhandisi Tarimo anaeleza pia hali ya barabara za lami zilikuwa ni kilomita 124.08, barabara za changarawe zilikuwa na urefu wa kilomita 1395.87 na barabara za udongo zilikuwa kilomita 5839.2 huku kukiwa na madaraja 91, kalavati 5398, boksi kalavati zilikuwa 496 na madaraja mfuto (drift) yalikuwa 202.

Mhandisi Tarimo anasema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, Serikali imeongeza bajeti ya TARURA Mkoa wa Tanga kutoka Sh bilioni 12.428 hadi kufikia kiasi cha Sh bilioni 37.815. 

“Ongezeko hili la bajeti sawa na zaidi ya asilimia 300, haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali hasa katika kuboresha barabara na miundombinu yake na kuwaondolea umasikini wananchi wa Tanga na Watanzania wote kwa ujumla.”

Anasema kutokana na ongezeko la bajeti ya matengenezo ya barabara, TARURA Mkoa wa Tanga umeweza kuimarisha na kuboresha barabara na miundombinu ambapo barabara za kiwango cha lami zimeongezeka kutoka kilomita 124.08 hadi kilomita 141.83.


Pia barabara za changarawe zimeongezeka kutoka km 1395.87 hadi km 1795.509, pia kupunguza kilomita za barabara za udongo kutoka 5839.2 hadi kilomita 5436.347.

“Na upande wa vivuko tumeweza kuongeza kutoka madaraja 91 hadi 100, daraja mfuto (drift) kutoka 202 hadi kufikia 306, kalavati 5019 hadi kufikia kalavati 5,398, boksi kalavati 428 hadi kufikia boksi kalavati 498".

“Haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha mtandao wa Barabara, kwa kipindi cha miaka miwili ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Awamu ya Sita,” anasema.

Anasema katika mwaka wa 2021/22, Serikali ilitenga fedha Sh bilioni 1.219 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika kijiji cha Msomera eneo ambalo Serikali imetenga kwa ajili ya kuwapokea wananchi kutoka Ngorogoro.

Mhandisi Tarimo anasema pia kazi kubwa imefanyika ya kufungua barabara kilomita 66.1, kuweka changarawe km 9 ujenzi wa boksi kalavati 1 na ujenzi wa daraja kubwa eneo la Mbagwi kazi zote zimeshakamilika. 


Anasema pia kazi ya awamu ya pili ya ufunguaji wa barabara ya km 103 na uwekaji wa changarawe km 22.4 unaendelea katika kijiji cha Msomera na Serikali imetenga Sh bilioni 1 na mkandarasi yupo anaendelea na kazi na tayari ameshafungua kilomita 30. 

Anasema kupitia fedha za tozo Serikali imetenga Sh bilioni 3.85 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mkomazi eneo la Kwasunga-Mswaha Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kazi ambayo imefikia asilimia 65 na inatarajia kukamilika Septemba 9 mwaka huu.

Akizungumzia mipango mikakati ijayo, Mhandisi Tarimo anasema kwa mwaka 2023/24 TARURA Mkoa wa Tanga imepanga kuendelea kuboresha na kufanya matengenezo ya barabara na vivuko ikiwa ni pamoja na kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 13.18 kwa kiwango cha lami hatua ambayo itaongeza urefu wa barabara za lami zilizopo kutoka kilomita 141.83 na kuwa kilomita 155.01.

Pia TARURA Mkoa wa Tanga umepanga kujenga barabara kilomita 723.414 kwa kiwango cha changarawe ambapo itaongeza barabara hizo kutoka kilomita 1,795.51 hadi kuwa kilomita 2,518.924 na ujenzi wa madaraja 9, madaraja mfuto 4, madaraja boksi kalavati 27 na makalavati 116. 

“Haya ni mafanikio makubwa kwa kipindi cha miaka miwili chini ya uongozi wa Mhe Rais Samia kwa Wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa ujumla.” 

Mhandisi Tarimo anaongeza: “TARURA Mkoa wa Tanga inapongeza hatua ya Rais Samia ya kutuongezea bajeti ya matengenezo ya barabara kwa zaidi ya asilimia 300, kutoka shilingi bilioni 12.428 hadi shilingi bilioni 37.815.”

“Hii haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu, kupitia kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara kuongeza fursa za ajira kwa Wananchi na kuwawezesha wanachi kufika kusikofikika kupata mahitaji na huduma za kijamii.

HONGERA NA ASANTE SANA MHE. RAIS WETU MPENDWA DR SAMIA SULUHU HASSAN! KAZI IENDELEE.’’

No comments:

Post a Comment