Asila Twaha, LINDI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Ofisi ya Rais –TAMISEMI kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa watendaji watakaobainika wamekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za utekelezaji wa miradi ya mendeleo .
Hayo yamebainishwa leo tarehe 24 Machi, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Halima Mdee (Mb) wakati wa majumuisho wa ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na Manispaa ya Lindi, Mkoani Lindi.
“hii sio tu kwa Halmashauri hizi za Mkoa wa Lindi hapa nazungumzia Halmashuri zote nchini watendaji wanaokiuka kufuata Taratibu, Sheria na Kanuni za utekelezaji wa miradi wachukuliwe hatua”amesisitiza Mhe.Mdee
Mdee ameishauri Ofisi ya Rais –TAMISEMI kushughulikia suala la ongezeko la watumishi katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwe na ufanisi na ubora wenye tija katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo hasa katika usimamizi wa miradi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema suala la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 watendaji wanatoa huduma hizo lakini pia hawafuati kanuni zilizopo kwenye utoaji wa mikopo kama inavyotakiwa na Serikali.
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anatimiza miaka miwili alisema asilimia kubwa ya mikopo hii inayotolewa hua hairudi hivyo ni wajibu wa Wakurugenzi kusimamia mikopo”amesema Mhe. Mdee
Ameishauri Ofisi ya Rais- TAMISEMI kuongeza kigezo cha urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 ambapo Serikali iliweka dhamira njema ya kuwasaidia wananchi lakini inaonekana dhamira hiyo inatumiwa vibaya.
Aidha, Kamati imeishauri Ofisi ya Rais- TAMISEMI miongoni mwa vigezo vya kupima ustadi wa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kiongezwe kigezo cha ufanisi wa Mkurugenzi katika kutoa mikopo na kufuatilia ipasavyo marejesho ya mikopo hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imewataka Wakurugenzi hao kutambua kuwa wameaminiwa na Rais Samia ili kumsaidia kwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kusimamia hivyo, ni vyema wakarekebisha dosari na madhaifu katika maeneo yao ili kuziletea Halmashauri maendeleo.
Kamati imawataka Wakurugenzi kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani angalau kwa asilimia 10% ya kiwango kinachokusanywa ili kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na ziweze kuleta tija katika maendeleo ya jamii.
Kamati imeitaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa nchi nzima kutathmini upya utaratibu wa Kisheria na muundo wa kitaasisi utakaowezesha usimamaizi na uendeshaji bora wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa Kitaifa.
Vilevile Kamati imewataka Wakurugenzi kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuwezesha Halmashuari hizo kutenga kiasi kilichopangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema, kwa mwaka wa fedha 2020/21 Manispaa ya Lindi ilitenga Tsh. 345 mil kati ya Tsh. 688 zilizopaswa kutengwa ikiwa ni 40% ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Kamati inaitaka Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria dhidi watakaobainika kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma.
Kwa upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi ameishukuru kamati ya LAAC na kuwahakikishia maelekezo yaliyotolewa na kamati yatafanyiwa kazi.
Mhe. Ndejembi amesema, kuhusu mikopo ya asilimia 10 Ofisi ya Rais –TAMISEMI imeshaunda mfumo wa asilimia 10 na vikundi vitasajiliwa ndani ya mfumo na mikopo hiyo itatolewa kwa wale waliojisajili kwenye mfumo huo.
Aidha, amesema kwa changamoto ya upungufu wa watumishi katika usimamizi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu hasa katika majengo ya utawala, hospitali na mashule kupitia “force account” ameeleza kuwa, Serikali imeshatoa kibali kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi cha kuajiri wahandisi 260 ambao wahandisi hao watapelekwa katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
“Ni kuhakikishie Mwenyekiti na wajumbe wote wa Kamati ya LAAC yale yote mliyotuelekeza Ofisi ya Rais –TAMISEMI tupo tayari tumeyapokea na kuyafanyia kazi na kuwasilisha taarifa yetu kwa maandishi” Mhe. Ndejembi
No comments:
Post a Comment