Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Hali duni ya Lishe husababisha kupungua kwa kinga ya mwili, kuongezeka kwa uwezekano wa kupata magonjwa, kupungua kwa tija katika uzalishaji mali na maendeleo kwa ujumla. Elimu ya Lishe kwa watoto wenye umri wa kwenda shule ni muhimu kwa sababu huongeza ushiriki wao katika kuhakikisha wanapata chakula bora na kuzingatia ulaji unaofaa.
Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Bi. Devotha Njalika wakati akitoa elimu ya Lishe kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Tamota iliyopo wilayani humo, Mkoani Tanga siku ya tarehe 21.03.2023.
Jumla ya Wanafunzi 370 katika shule hiyo wamepatiwa elimu ya lishe iliyotolewa sambamba na tathmini ya lishe kwa kupima uzito na urefu wa wanafunzi.
Akiongea na wanafunzi hao, Bi. Devotha alisema " mnapaswa kuzingatia ulaji unaofaa ikiwemo kula mbogamboga na matunda mbalimbali kwa wingi, ili kuimarisha afya zenu na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa, hivyo mtakuwa na mahudhurio mazuri darasani na kuinua kiwango cha ufaulu wenu"
Halikadhalika, wanafunzi 2305 wamepewa elimu ya jinsi ya kuandaa bustani za mbogamboga na matunda kutoka shule nne zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Kigoma ambazo ni Sekondari ya Kasimbu, Buhanda, Kigoma na shule ya msingi buhanda. Elimu hiyo imetolewa kuanzia tarehe 20 hadi 22 Machi, 2023, ikihusisha kuunda klabu za lishe katika shule hizo.
Akizungumza na wanafunzi pamoja na walimu katika mojawapo ya shule hizo, Bw. Edward Chikoma kutoka asasi ya ANUE alisema "suala la utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni linapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote ikiwemo wadau wa wa maendeleo, Asasi za kiraia, wazazi na walezi, kamati za shule, walimu na wanafunzi wenyewe"
"kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda sheleni hurahisisha upatikanaji wa chakula na hufanikisha utoaji wa mlo kamili kwa wanafunzi pindi wakiwa shuleni" Bw. Chikoma aliongeza.
Ikumbukwe juhudi zote hizi zinafanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na Lishe katika shule za msingi hadi kidoto cha nne, Nchini.





No comments:
Post a Comment