WANAWAKE WATAKIWA KUNUSURU MAADILI YA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, March 5, 2023

WANAWAKE WATAKIWA KUNUSURU MAADILI YA JAMII


Na Mwandishi wetu Kongwa

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kongwa Bi. Joyce Ibrahim Mkaugala amewataka wanawake kunusuru maadili ya jamii ambayo kwa kiasi kikubwa yamemomonyoka.

Mkaugala amesema wanawake wanalo jukumu kubwa la kusimamia maadili ya jamii kwa kuhusika kikamilifu kwenye malezi ya watoto sanjali na kuhakikisha wanakwenda shule.


Bi. Joyce amesema hayo katika hafla fupi ya kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya wanawake duniani, iliyoandaliwa na Divisheni ya Maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na umoja wa walimu wanawake Wilaya ya Kongwa, na kufanyika Machi 4, 2023 katika Kata ya Mkoka.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Dkt. Omary A. Nkullo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, aliwataja wanawake kama watu wenye nguvu kubwa katika kusimamia mchakato wa Maendeleo.

Dkt. Nkullo, ametolea mfano kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwanamke, ambaye katika Kipindi cha utawala wake, Serikali imetekeleza miradi mingi ya Maendeleo katika Sekta mbalimbali zikiwemo Afya, Elimu na miundombinu.


Katika hafla hiyo, Dkt. Nkullo alikabidhi vifaa mbalimbali vya Usafi wa mwili na vyombo vya chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya Msingi Mkoka vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane vilivyotokana na michango ya umoja wa walimu wanawake Wilaya ya Kongwa na wadau mbalimbali.

Afisa Elimu, Elimu maalum Bibi. Sophia Mohamed licha ya kutoa Shukrani zake kwa Divisheni ya Maendeleo ya jamii na umoja wa walimu wanawake, pia amesisitiza jamii kupaaza sauti kupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto wakiwemo wenye mahitaji maalum.


Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Bibi. Paskalina Duwe amepongeza mshikamano wa umoja wa walimu wanawake na amewaomba kuendelea kusaidia makundi mengine ngazi ya jamii kama wanavyofanya kwa wanafunzi.

Bibi Duwe ametumia fursa hiyo kutoa wito wa kushiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani ambayo Kimkoa itafanyika Wilayani Kondoa.


Naye Mhe. Catherine Mapuga Diwani Viti Maalum Kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Mkoka, amewapongeza waandaaji wa hafla hiyo.

Akifunga mkutano wa hafla hiyo, mwenyekiti wa kijiji cha Mkoka Bwana Eliah Chibago alihimiza wanawake kukemea vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyotajwa kukithiri baina ya wanawake na wanaume.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Kata ya Mkoka Kwa kufanya Usafi wa Mazingira na kuwatembelea Watoto wenye mahitaji maalum.

No comments:

Post a Comment