Na Okuly Julius-Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt.Selemani Jafo ameziagiza Secretariet za mikoa, Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya zote nchini kuendelea kudhibiti matumizi ya vifungashio visivyoruhusiwa kisheria kwa kuzingatia kuwa Utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ni jukumu la wadau wote.
Dkt.Jafo ametoa agizo hilo leo Aprili 6,2023 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki , ambapo amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa kushirikiana na Sekretariati za Mikoa kupitia Ofisi zote za kanda za NEMC kuendesha Kampeni za kuondosha mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.
Pia ,Dkt.Jafo amesisitiza na kutahadharisha umma kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio hivyo kuwa mifuko ya kubebea bidhaa, na kwa mujibu wa sheria, adhabu stahiki zitatolewa kwa wanaokiuka sheria wakiwemo watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa.
"Tarehe 26 Agosti, 2022, nikiwa kama Waziri mwenye dhamana ya mazingira nilitoa taarifa kwa umma kuendelea kusisitiza marufuku ya matumizi ya vifungashio kutumika kama vibebeo hususan kwa bidhaa za masokoni,"
Nq kuongeza kuwa "Hali hii inaonesha ukiukwaji mkubwa wa Kanuni ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki unaofanywa na baadhi ya wazalishaji na wasambazaji ambao wamebadilisha mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa. Hii ni kinyume na kanuni ya 8 ya Kanuni tajwa hapo juu,"amesisitiza Dkt.Jafo
Ikumbukwe kuwa tarehe 1 Juni, 2019, Serikali ilipiga Marufuku Uzalishaji; Uingizaji nchini, Usafirishaji nje ya nchi; Usambazaji; na Matumizi ya mifuko ya plastiki. Mafanikio ya marufuku hii yamewezesha kuimarika kwa hali ya usafi wa mazingira hususan maeneo ya mijini sambamba na kuongezeka kwa matumizi ya mifuko mbadala ikiwemo non-woven na mifuko ya karatasi; na fursa za ajira kwa wazalishaji wa mifuko mbadala.
No comments:
Post a Comment