Na Mwandishi wetu Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi , ambaye pia ni mlezi wa Timu za Uchukuzi Bwana Gabriel Migire ameahidi kuendelea kutoa ushawishi wa kisekta katika kuwapa sapoti zote zinazostahili watumishi wanaowakilisha Taasisi za Uchukuzi kwenye michezo mbalimbali katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea Mkoani Morogoro.
Bwana migire ameyasema hayo leo alipozitembelea timu zinazowakilisha Sekta ya Uchukuzi kwenye michezo mbalimbali ya mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea Mkoani Morogoro ambapo pia alipata fursa ya kushuhudia mchezo wa kukata na shoka wa mpira wa miguu kwa upande wa wanaume kati ya Uchukuzi sports club na Moro Dc uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo cha Ujenzi ambao ulimalizika kwa timu ya Uchukuzi kuibugiza Moro Dc kwa magori 2 kwa 1.
“Mimi kama Kiongozi kwenye eneo la Uchukuzi nitaendelea kufanya ushawishi kwa njia mbalimbali kuhakikisha timu hizi za Sekta ya Uchukuzi zinapokuwa zinakuja kwenye mashindani mbalimbali yakiwemo haya ya Mei Mosi zinapewa sapoti ya hali ya juu na siyo bajeti ya kushtukiza na nawahakikishia tutakuwa tumeshajipanga na sisi tunachokitaka kutoka kwenu ni nguvu zenu tu na mkacheze kama ndugu lakini sapoti ya Serikali mnayo” amesisitiza Migire
Vile vile Katibu Mkuu Migire amewahakikishia viongozi na wachezaji wa Timu za Uchukuzi kuwa atahakikisha kila mechi kuwe na kiongozi wa Wizara kikubwa na kushirikishana ratiba ili kama Taasisi waone ni jinsi gani watasapoti Timu za Uchukuzi na siku ile ya mwisho kabla ya Mei Mosi Wakuu wote wa Taasisi na yeye mwenyewe watajipanga wawepo.
Akimkaribisha katibu Mkuu, mwenyekiti wa Klabu ya Uchukuzi Bwana Andrew Magombana amesema timu zote zinazowakilisha Sekta ya Uchukuzi kwenye michezo ya Netiball, Volley ball, kuvuta kamba, mpira wa miguu, riadha, michezo ya jadi kama bao, draft na karata kwa upande wa wanawake na wanaume zimejiandaa vyema na zilifika mkoani Morogoro kwa wakati na mpaka sasa zinaendelea kufanya vizuri sana na tunauhakika tutafanya vizuri zaidi kwenye mashindano haya na hata kuivunja rekodi yetu ya mwaka uliopita.
Naye Meneja wa Timu ya Klabu za Uchukuzi Ndugu Gabriel Samson amesema timu zote kwa upande wa wanawake na wanaume zinaendelea vizuri na zimepata maradhi mazuri japo kuna changamoto za majeruhi kwa baadhi ya wachezaji kwa upande wa wanawake na wanaume lakini wanaendelea na matibabu na hali zao zinazidi kuimarika.
Kwa upande wake Mwalimu wa timu ya Mpira wa miguu ya Uchukuzi Bwana Athuman amesema mchezo ulikuwa mgumu na hali ya mvua za rasha rasha zinazoendelea mkoani Morogoro zinazidi kuleta ugumu kwa wachezaji lakini umakini kwenye mazoezi, nidhamu na kujituma kwa wachezaji ndani ya uwanja vimesaidia kuibuka na ushindi.
Michezo ya Mei Mosi Mwaka huu 2023 inayowahusisha Watumishi wa Umma na Sekta binafsi iliyoanza tarehe 16 Aprili,2023 Mkoani Morogoro inapambwa na kaulimbiu”Miaka miwili ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Imeimarisha Michezo na kuongeza Ufanisi Kazini, Kazi Iendelee” inatarajiwa kufikia tamati tarehe 29 Aprili 2023.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano,Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment