WAKRISTO 6147 WAFIKIWA NA ELIMU YA UGONJWA WA MARBURG KATIKA IBAADA YA JUMAPILI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 3, 2023

WAKRISTO 6147 WAFIKIWA NA ELIMU YA UGONJWA WA MARBURG KATIKA IBAADA YA JUMAPILI.


Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Ikiwa Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ikiendelea na juhudi mbalimbali za uelimishaji katika mkoa wa Kagera juu ya Ugonjwa wa Marburg, jumla ya waumini 6147 kutoka makanisa mbalimbali ya Kikristo Bukoba mjini na Wilaya ya Biharamulo wamefikiwa na elimu hiyo wakiwa katika sehemu za ibaada ya kawaida ya siku za Jumapili.


Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Kengele tatu Bukoba Mjini ni miongoni mwa makanisa yaliyofikiwa na Waumini wake kupatiwa elimu ya Ugonjwa wa Marburg kukiwa na takriban jumla ya waumini 3019 walionufaika na elimu ambapo mwakilishi kutoka Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga, Elimu ya Afya kwa Umma Beauty Mwambebule amehimiza washiriki kuendelea kuepuka tabia zinazoweza kuchochea maambukizi ya Marburg.


"Tuepuke vitendo vinavyoweza kuchangia Maambukizi, kutosalimiana kwa kushikana mikono,tunawe mikono Kwa maji safi na tiririka na sabuni hasa ya maji, tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima, tukae Kwa kuachana nafasi, tunapoona dalili za ugonjwa huu kama vile kutokwa na damu Sehemu za wazi ,homa isiyo ya kawaida piga bure kwa namba 199 lakini tumshukuru Mungu hali sasa inaendelea vizuri hakuna Maambukizi mapya" amesema Beauty Mwambebule.


Halikadhalika, Kanisa la KKKT Usharika wa Kashura Bukoba jumla ya waumini 625 Wamefikiwa na Elimu ya ugonjwa wa Marburg ambapo Mchungaji wa Usharika wa Kashura Mch.Alex Kasisi ameishukuru Wizara ya Afya kwa kusema"Nashukuru sana Wizara ya Afya kwa kujali Afya za watu na kuamua kutembelea Kanisa letu kutoa ujumbe huu Mahsusi kuhusu ugonjwa huu wa Marburg, sisi kama kanisa hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha ujumbe huu unafika Kwa kila mshiriki"amesema .



Katika Kanisa la TAG Hamugembe Bukoba Mjini jumla ya waumini 852 wamefikiwa na elimu ya tahadhari juu ya Ugonjwa wa Marburg, jinsi unavyoenezwa na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambapo Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo Mch.Erasto Kyando amesema wao kama viongozi wa dini wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano ya ugonjwa huo .


"Tuendelee kumwomba Mungu aingilie kati juu ya Ugonjwa huu , sisi kama kanisa tupo tayari kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika mapambano ya ugonjwa wa Marburg na nashukuru sana jitihada zinazoendelea kufanywa na Wizara ya Afya " amesema Mch.Erasto Kyando .


Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Penford Joel amehimiza umuhimu wa kuripoti katika mamlaka husika pindi panapohisiwa kuna mtu ana maambukizi.


 "Kama kama kuna mtu yeyote anahisiwa anadalili za ugonjwa ni vyema kuripoti katika Mamlaka ya Serikali za mitaa Ili huduma ya Msaada wa haraka ufanyike "amesema .


Aidha, Penford ameongeza kuwa "Tuepuke Tabia ya kugusa maeneo tofauti tofauti kama hakuna ulazima kwani unaweza ukagusa Sehemu ambapo mwenzako amegusa na pana Maambukizi ya ugonjwa huo" amesema 

Pia, jumla ya waumini 327 Kanisa la EAGT Kahororo, Mlima wa Ahadi Bukoba Mjini wamefikiwa na kupewa elimu juu ya Ugonjwa wa Marburg.

 
Nao baadhi ya waumini wa makanisa mbalimbali ya Kikristo akiwemo Mwalimu Shukuru Kyaka kutoka Kanisa la KKKT Kengele tatu Bukoba mjini pamoja na Anchila Mkela wamesema hatua za Wizara ya Afya kuongeza nguvu ya uelimishaji itasaidia wananchi kuwa na uelewa Zaidi huku wakitoa ushauri kuongeza wigo hasa katika kuwaelimisha wananchi kuepuka misururu na misongamano mikubwa hasa kwenye misiba.

 
Mbali na makanisa mbalimbali ya Bukoba Mjini kufikiwa elimu baadhi ya makanisa yaliyopo Wilaya ya Biharamulo yamefikiwa na kutolewa ujumbe mahsusi kuhusu Marburg ikiwa ni pamoja na Kanisa la Roma Catholic (RC) Kigango kata ya Kitendaguro huku Waumini 895 wakipata elimu hiyo, Kanisa la AICT Biharamulo na jumla ya waliofikiwa ni 128,watoto 63 na watu wazima 65 ,Kanisa Katoriki Biharamulo idadi ya waumini 310 wamepokea elimu juu ya ugonjwa wa marburg.


Makanisa mengine ni pamoja na Kanisa la T.A.G Biharamulo ambapo jumla ya waumini 207 wamefikiwa huku KKKT Biharamulo ambapo jumla ya waumini 94 wamepata elimu juu ya ugonjwa wa mlipuko wa Marburg huku kanisa la FPCT Biharamulo maendeleo parish nao wakinufaika na elimu hiyo.


 Ikumbukwe kuwa timu ya wataalam wa Afya kutoka Wizara ya Afya wameweka Kambi mkoani Kagera kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzunguka maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko wa watu kwa kushirikiana na watalaam wa afya ngazi ya jamii hadi mkoa na kutoa elimu kwa njia ya vipindi kupitia Redio Jamii zilizopo mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment