WAZIRI MHAGAMA NA SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 7, 2023

WAZIRI MHAGAMA NA SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akimkabidhi nyaraka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati yao. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Aprili 06, 2023 Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo (hawapo pichani) wakati wa makabidhiano ya Ofisi kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Baadhi Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakimsikiliza Waziri wa Nchi Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kumkaribisha mara baada ya kuwasili Ofisini hapo.
Mwandishi Mwendesha Ofisi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi.Tusekile Mwakang’ata akimkabidhi ua Waziri wa Nchi Ofisi hiyo Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) alipowasili mara baada ya kuwasili katika Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi walioshiriki hafla ya makabidhiano, kushoto kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais UTUMISHI Mhe. Ridhiwani Kikwete baada ya makabidhiano hayo.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)



Na Mwandishi wetu- Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


Ameyasema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano kati ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya uteuzi uliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Aprili 01 mwaka 2023.


Waziri Mhagama amesema dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuwahudumia wananchi mahali na kwa nafasi yoyote anayopangwa kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizopo.


“Mara zote dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha kila unapopangwa unafanya kazi kwa nguvu zako zote pamoja na utii na kuwa tayari kutumikia Taifa mahali popote kwahiyo kurudi kwangu hapa najihesabu ni sehemu yenu pia kama mtumishi wa umma,” Amesema Mhe. Jenista.


Pia amebainisha kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi wake watashindwa kujidhatiti na kufanya kazi kwa moyo kwa kuzingatia mazingira husika.


“Msingi wa tija katika utendaji wa kazi Serikalini unatutaka kuwa na uratibu mzuri unaozingatia sera, miongozo na kanuni zilizopo kwa kuzingatia jukumu kubwa la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli zote za Serikali na tuna jukumu la kusimamia Bunge kama mhimili mwingine ndani ya Nchi hivyo bila kuwa na ushirikiano hatutafikia malengo tunayokusudia,” Ameeleza.


Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa fursa ya kulitumikia Taifa pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.


“Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini kuendelea kuwatumikia wananchi katika nafasi hii na watumishi pia nawashukuru kwa ushirikiano mlionipatia na kuwezesha kufanikisha shughuli za uratibu kwa kipindi chote,” Ameshukuru Mhe. Simbachawene.


Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Mhe. Simbachawene kwa utumishi wake mwema katika Ofisi hiyo.


Aidha ametumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Waziri Mhagama katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananachi.

No comments:

Post a Comment