NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Wananchi wawili wa wilaya ya Ngorongoro wamekata rufaa ya Jinai namba 9 ya 2023 inayopinga utozaji wa faini shilingi 100,000 kwa ng’ombe na shilingi 25000 kwa Mbuzi na kondoo jambo lililotendeka januari 25,2023 baada ya mifugo yao kukamatwa ambao ni ng'ombe 130, Mbuzi na Kondoo 80 kukamatwa katika pori la akiba la Paloteti lililopo wilayani humo.
Rufaa hiyo iliyotajwa mbele ya Jaji Mohamed Gwae katika mahakana kuu Kanda ya Arusha imepangwa kusikilizwa Mei 10,2023 huku walalamikiwa wakiwa ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mkurugenzi wa wanyamapori pamoja na Jamhuri ambapo wananchi hao wanapinga utozaji wa faini hiyo pamoja na mamlaka ya aliyetoza faini ambapo upande wa wajibu rufaa iliwakilishwa na wakili wa serikali Tonny Kilomo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama wakili upande wa waleta maombi Denis Mosses alisema kuwa mifugo hiyo ambayo ni ngombe 130 mali ya Baraka Keisoi na Mbuzi na Kondoo 80 mali ya Raphael Oloishiro ambapo kila ng'ombe alitozwa faini ya shilingi 100,000 na jumla kuwa milioni 13,000,000 huku Mbuzi na Kondoo wakitozwa shilingi 25 na jumla kuwa milioni 2,000,000.
Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori kiwango ambacho kinatarajiwa kutozwa kwa mtu ambaye ameigiza mifugo kwenye pori la akiba atalipa faini kuanzia laki tatu na isizidi milioni tano ambayo hulipwa kwa kosa na siyo kwa ng'ombe mmoja mmoja kwasababu wanyama hawatendi kosa bali ni mtu ndiye anayetenda kosa.
Aidha amefafanua kuwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro haina mamlaka kisheria ya kutoza faini kwenye maeneo yaliyo nje ya hifadhi ya mamlaka hiyo na hiyo ni kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mamlaka hiyo inaonyesha kuwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itakuwa na mamlaka kwenye maeneo yaliyo ndani ya mipaka ya hifadhi yake.
“Sheria ya wanyama pori imeweka wazi kuwa mkurugenzi wa wanyamapori ndiyo anayesimamia mapori ya akiba pamoja na mapori tengefu hivyo NCAA kukamata na kutoza faini hiyo ni kinyume cha sheria kwani hawana mamlaka ya kufanya hivyo lakini pia hawakutoza faini kwa mtu aliyetenda kosa bali kwa kichwa cha Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo ambayo hiyo pia ni kinume cha sheria,” Amesema wakili huyo.
Hata hivyo hoja ya msingi ya waomba rufaa wawili ambao ni wakazi wa Ngorongoro ni utozaji wa faini ya shilingi 100,000 kwa kichwa cha ng’ombe ni batili na ni kinyume cha sheria, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) haina mamlaka ya kutoza faini kwenye sehemu ambazo zimeanzishwa na Sheria ya Wanyama pori, Sura 283 ambayo mwenye mamlaka ni mkurugenzi wa wanyamapori, Kutoza faini ya shilingi 25,000 kwa kondoo na mbuzi ni batili na ni kinyume cha sheria pamoja na Kutoza faini ya 13,000,000 ni kinyume cha kiwango kilichowekwa na sheria.
No comments:
Post a Comment