OR - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali kupitia Mradi wa Kuimarisha Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) imepeleka shilingi milioni 940.9 katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara kwa ajili ya kuboresha elimu ya Awali na Msingi.
Ameeleza hayo tarehe 07 Mei, 2023 wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Bisarara Wilayani Serengeti wakati alipoambata na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeo ya Makazi na Naibu Waziri Maliasili na Utalii kusikiliza na kutatua kero za wananchi Mkoani Mara.
“Mradi huu wa BOOST unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, utagharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.15 ambapo katika kipindi hiki cha mwezi wa tano tayari Halmashauri ya Wilaya ya Serrngeti imeletewa shilingi milioni 940.9 kuboresha elimu ya awali na msingi ” amesema Waziri Kairuki.
Kairuki amesema katika fedha hizo za Mradi wa BOOST, shilingi milioni 540.3 zitatumika kujenga shule ya Msingi Mapinduzi B yenye mikondo miwili katika kata ya Mugumu, milioni 300 zitajenga vyumba vya madarasa 12 katika shule za Kambarage, Kisaka, Mapinduzi, Monunu na Remung’oroti na shilingi milioni 69.1 zitajenga madarasa mawili ya awali shule ya Remung’oroti.
Ameendelea kufafanua kuwa shilingi milioni 31.5 zitajenga matundu ya vyoo 15.
Aidha, Waziri Kairuki amesema shilingi milioni 470 kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ililetwa katika Wilaya Serengeti kujenga shule ya Sekondari Mpya ya Morotonga ambayo wanafunzi zaidi ya 80 wameshaanza masomo katika shule hiyo.
Waziri Kairuki amesema, shilingi milioni 600 italetwa katika Kata ya Nagusi kujenga shule mapya ya kata ambazo zitaletwa katika awamu mbili, ambapo awamu kwanza italetwa milioni 470 na awamu ya pili milioni 130 itajenga nyumba ya waalimu na kununua vifaa vya Tehama.
No comments:
Post a Comment