Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ,Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaelekeza Askari wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini kuanza zoezi la kusaka fisi wanaovamia makazi ya watu katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Cecilia Pareso aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuvuna fisi wanaovamia makazi ya watu katika Kata ya Endamarariek Wilayani Karatu
‘Niendelee kuelekeza kuanzia sasa Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kaskazini waelekee Karatu wakaanze kufanya msako wa fisi hao ili wananchi waweze kuona umuhimu wa uhifadhi lakini pia fisi hao waweze kurudishwa hifadhini” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Mhe. Masanja amesema kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza programu ya kuelimisha wananchi namna bora ya kujikinga wa wanyama wakali na waharibifu.
Amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Jeshi la Uhifadhi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imevuna fisi saba (7) waliovamia makazi ya wananchi ili kunusuru wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu dhidi ya kujeruhiwa na kuuawa na fisi hao.
“Tangu mwaka 2019 hadi sasa jumla ya fisi saba wamevunwa na pia Serikali imekuwa ikifanya msako wa fisi mara kwa mara katika maeneo husika” Mhe. Masanja amesisitiza.
Aidha, ameongeza kuwa katika zoezi la kuvuna fisi hao jumla ya mapango/makazi ya fisi 11 yameharibiwa huku akisisitiza kuwa Jeshi la Uhifadhi linaendelea kufanya doria ili kuyabaini makundi ya fisi yaliyosalia na kuyavunja ikiwa ni pamoja na kuharibu makazi yao.
Kuhusu changamoto ya mamba katika ukanda wa Ziwa Victoria, Mhe. Masanja amesema Wizara imeshaanza programu ya kuwakinga wananchi na mamba kwa kujenga vizimba vya kuchotea maji ili wananchi wachote maji katika maeneo yaliyoainishwa tu.
Pia, amewaasa wananchi kuacha mazoea ya kuogelea kando ya Ziwa Victoria ili kuepukana na madhara ya kuliwa na mamba.
No comments:
Post a Comment