Na Okuly Julius-Dodoma
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka wazi kukamilika kwa Rasimu ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na kuamua kutoa rasimu hadharani ili kupata maoni ya mwisho hadi kufikia Mei 31, 2023.
Hayo yameelezwa Mei 9, 2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa Mkutano na waandishi wa Habari ambapo rasimu ya Mitaala mipya ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya uwaalimu inayokidhi Maelezo ya Mheshimiwa Rais nayo imekamilika.
"Mwanzoni tulipokea maoni bila kuwa na rasimu tukayachambua na kufanyia kazi, tumeyachakata maoni hayo, tukafanya uchambuzi wa kitaalamu, tumejifunza kutoka nchi mbalimbali na tumetengeneza Rasimu, sasa Umma wa Watanzania utaziona Rasimu hizi ili watolee maoni kwenye rasimu ambazo baada ya kuzingatia maoni tutaingiza kwenye michakato ya maamuzi". Alisema Prof Mkenda
Aidha alisema Wizara imeandaa semina na kongamano mbalimbali ya kuwapitisha wadau katika rasimu hizo, ikiwemo semina kwa wabunge wote kupitishwa kwenye rasimu hizo za mapitio ya sera na Mitaala mipya itakayofanyika kesho Mei 10, 2023.
Pia Prof. Mkenda alisema kuwa, wanaotaka kuhudhuria kongamano hilo wanakaribishwa kujisajili ikiwa tangazo la kualika ili kujisajili litatolewa leo na utaratibu wa kujisajili utatangazwa lakini wapo wataalam na wadau mbalimbali ambao wamepewa mwaliko rasmi hivyo wizara itajitahidi kutangaza kongamano hilo ili kila mtu asikilize maoni yanavyotolewa.
"Watanzania wote popote walipo wanakaribishwa kupitia rasimu hizi na kutoa maoni zao, Rasimu hizi zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Tovuti ya Idara ya Habari Maelezo, na Tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania”.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo alisema mialiko hiyo ipo ndani na nje ya Tanzania ambapo Watanzania wanaoishi nje ya nchi, wamealikwa na kutakua na utaratibu maalumu wa kushiriki mjadala huo na kutolea maoni.
"Watanzania wenzetu walioko nje ya nchi watatusaidia kujua kuna nini na watatoa maoni namna ya kuboresha Mitaala hii na sera hii kutokana na uzoefu wao wa nchi nyingine". Alisema Prof. Nombo
Na Kuongeza "Watanzania wote popote walipo wanakaribishwa kupitia rasimu hizi na kutoa maoni zao, Rasimu hizi zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia www.moe.gi.tz, Tovuti ya Idara ya Habari Maelezo www.maelezo.go.tz, na Tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania www.tie.go.tz.
Hata hivyo Mei 12 hadi 14 mwaka huu katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kunatarajiwa kufanyika kongamano la kitaifa la wadau wa elimu kuhusu uhuishaji wa sera na mitaala ya elimu ambapo wadau watakutana kujadili rasimu za sera za Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na mitaala mioya ya elimu ya awali, msingi, sekondari na Ualimu.
No comments:
Post a Comment