Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Doroth Gwajima ametoa rai kwa viongozi wa umma nchini kuzingatia maadili kwa kuwafundisha vijana maadili mema ili kuokoa kizazi kijacho.
Amesema, “lazima sisi viongozi tuwe mstari wa mbele kuwafundisha maadili mema vijana wetu ili kuwaepusha kudumbukia kwenye vitendo vinavyokinzana na maadili yetu ukiwemo ushoga na mapenzi ya jinsia moja.”
Dkt. Gwajima ametoa rai hiyo jijini Arusha Mei 4, 2023 alipokutana na baadhi ya viongozi wa mkoa huo walioudhuria mafunzo ya siku moja kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma. Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema, “tujiulize tunafanya nini kujenga kizazi bora katika taifa letu, lazima tuzingatie maadili yetu. Agenda ya maadili sio ya utumishi wa umma au nyinyi viongozi peke yenu, ni agenda ya wananchi wote.”
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Bw. David Lyamongi, Katibu Tawala Msaidizi Utawala mkoa wa Arusha kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo.
Akifungua mafunzo hayo, Bw. Lyamongi ametoa wito kwa wakuu wote wa taasisi mkoani humo kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wanapotimiza majukumu yao ili kujenga imani ya Serikali kwa wananchi na kuwasaidia wananchi kunufaika na rasilimali za nchi.
Alisema, “wakuu wote wa taasisi katika mkoa wetu lazima wawe na maadili yanayoeleweka ili wananchi wanufaike na mipango ya Serikali.”
Kwa mujibu wa Bw. Lyamongi, uadilifu wa viongozi wa umma unatakiwa kuwanufaisha wananchi kwa kupata huduma bora katika maeneo yao.
“Maadili ya kiongozi wa umma yanatakiwa kujidhihilisha mahali popote, kiongozi wa umma anapokuwa ofisini, mtaani au ndani ya familia yake, lazima awe mfano kwa jamii iliyomzunguka.
Katika hatua nyingine, Bw. Lyamongi ameagiza watendaji wakuu katika taasisi mbalimbali za mkoa wa Arusha kutoa miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya utumishi kwa watumishi walioko chini yao ili iwasaidia kujua mabadiliko ya kiutumishi.
“Ni vizuri mkatoa miongozo inayotolewa na Serikali kuhusu mabadiliko mbalimbali yakiwemo maslahi ya watumishi ili kuwasaidia watumishi kujua mabadiliko husika katika utumishi wa umma,” amesema.
Kwa upande wake Bi. Anna Mbasha, Katibu Msaidizi, Kanda ya Kaskazini ametoa wito kwa watoa maamuzi kuzingatia maadili katika kufanya maamuzi ikiwemo kupima madhara ya uamuzi wanaoufanya kwa umma.
Aidha, Bi Mbasha amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kutumia vibaya madaraka yao kwa kuendekeza tamaa na kuwanyanyasa watumishi walioko chini yao.
Amesema kuwa ni lazima kiongozi wa umma aepuke kuweka shinikizo dhidi ya mtumishi aliyeko chini yake anaposhughulikia mambo ya kiutumishi.
“Kiongozi wa Umma anatakiwa kuepuka shinikizo lisilofaa kwa mtumishi aliyeko chini yeke anapochukua hatua za kinidhamu au kumpandisha daraja badala yake, atumieni njia sahihi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi,” amesema.
Naye Bw. Fabian Pokela, Katibu Msaidizi toka Makao Makuu, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dodoma ameeleza kuwa miradi ya Taifa ya kimkakati kutosimamiwa vizuri kunatokana na baadhi ya viongozi wanaohusika na miradi hiyo kukosa uadilifu.
Bw. Pokela amesema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Mgongano wa Maslahi.
“Tatizo hili lina madhara makubwa kwa jamii ikiwemo miradi ya kimkakati kutokamilika ipasavyo na kwa wakati,” amesema.
Bi. Emmanuela Kaganda, Mkuu wa wilaya ya Arumeru akiongea kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwasababu wengi wetu tuna mamlaka makubwa katika maeneo yetu ya kazi na wapo viongozi waliopata ajali za kikazi sio kwasababu hawana uwezo wa kazi, bali ni kutokana na kuyakosa mafunzo hayao.
“Baada ya mafunzo haya, kila mtu aende na kusimama kwenye nafasi yake na atende haki,” alisema.
No comments:
Post a Comment