Na Gideon Gregory Dodoma
Afisa Afya Mkoa wa Dodoma Nelson Rumbeli amewataka wakazi wa Dodoma kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kufanya usafi wa MAZINGIRA ili kuhakikisha mkoa huo unaendelea kuwa katika hali ya usafi.
Rumbeli ameyasema hayo leo Mei 6,2023 wakati akishiriki zoezi la kufanya usafi na baadhi ya wafanya biashara walioko katika kituo cha Mabasi CBE Jijini Dodoma.
Amesema elimu ya usafi inatakiwa kupelekwa kwa wananchi wote ili kuweza kuepukana na magonjwa mbalimbali ya milipuko yanayoweza kujitokeza,kuboresha muonekano wa maeneo yao na kuwafanya watu wanao kuja kufanya shughuli za kiserikali kuuona mkoa huo kama sehemu muhimu sana ya kufikia pamoja na kufanya majukumu yao.
“Kwa mfano leo tumefanya ukaguzi kwa maana kupita kaya kwa kaya kukagua usafi na mwitikio wa wananchi ulikuwa mzuri, tunachohitaji ni chachu ya maana serikali za mitaa hasa hapa halmashauri ya Jiji kwa maana ya kuogeza msukumo wa kusimamia,”amesema.
Aidha ameongeza kuwa katika ukaguzi huo amegunduwa kuwa changamoto kubwa ni mfumo wa usimamizi wa kusimamia kwamaana watendaji wa mitaa kutokuwepo katika maeneo yao na kuomba eneo hilo kufanyiwa kazi na viongozi wa mitaa, mtendaji wa mtaa, mtendaji wa Kijiji na afisa afya ngazi ya kata.
“Zoezi hili litakuwa endelevu kama nilivyokwisha kusema hapa Dodoma ni makao makuu ya nchi na kama tunayo kampeini ya “PENDEZESHA DODOMA” kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao kimsingi tunashirikiana nao wanafanya kitu kizuri hasa kushiriki katika shughuli hizi za kiserikali,”amesema.
Amesema usafi ni moja kati ya kitu kikubwa cha kukabiliana na milipuko ya magonjwa, na swala hilo ni kipaumbele cha mkoa na nchi.
Kwa upande wake Mkurungenzi wa kampuni Ya Mazingira ya MAKAMBUYA ENVIROMENTAL Co. LIMITED,William Machimu amezungumzia malengo ya Kampuni hiyo katika kuhakikisha mazingira yanakuwa katika hali ya usafi amesema malengo yao wameyagawanya katika makundi mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwamba watu kwani wasipoeleweshwa na kupata elimu iliyo sahihi hawezi kufikia malengo na matarajio ambayo yameyakusudia.
“Kwa hiyo tuna mpango wa kutoa elimu katika makundi mbalimbali hususani tumeyaainisha kwenye uzinduzi utakao kwenda kufanyika tarehe 25 ,Mei 2023, ambapo tutawakutanisha bodaboda, mama lishe, wafanya biashara, mabenki na vituo vya magita pamoja na makundi mbalimbali tutakayo yazindua kwa AJILI ya kutoa elimu, lakini malengo yetu yatachuku muda wa miaka miwili hadi mwaka 2025,”amesema.
Pia ametoa ushauri kwa wananchi ambapo amewashauri kuchukua nafasi wao wenyewe kuweza kuangalia ni namna gani wasitupe taka ovyo kwa vifaa vinavyo maliza muda wake.
“Kwenye maandalizi yetu baada ya uzinduzi tutaweka vifaa vya kutupia taka kila eneo la mita chache ili mtu anapomaliza kutumia vifaa vinavyo maliza muda waweke kwenye vifaa vya kutupia taka, ambapo hata serikali pamoja na wadau mbalimbali, wananchi pamoja na ofisi ya mkuu wa Mkoa, ofisi ya mkuu wa wilaya pamoja na ofisi ya mkurugenzi watuunge mkono juhudi hizi ambazo kampuni imeamua kufanya,”amesema.
Akizungumza baada ya zoezi hilo la usafi Elias Mkwawa mkazi wa Makole amesema wao kama vijana wamejitoa kwaajili ya kulipendezesha Jiji la Dodoma na kuweka mikakati ya kufanya usafi kila baada ya siku Tatu na kuweza kununua vifaa vya kuhifadhia taka kupitia umoja wao.
“Sisi kwa upande wetu mpaka sasa tulikuwa na changamoto ya vifaa vya kuhifadhia taka na vyoo vya kulipia hivyo tunashukuru kupitia uongozi tulio nao mpaka sasa changamoto hizo tayari zimetatuliwa na kila mtu kwa sasa ni mlinzi wa mwenzake akiona mtu anatupa taka hovyo anachukuliwa hatua za kisheria,”amesema.
Pia, Mkwawa ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kufanya usafi na kupitia uongozi wa mtaa wa Makole wale watakao kataa kushiriki katika zoezi hilo kuchukuliwa hatua kwani suala la usafi sio la mtu mmoja ni la kila mtu.
Naye Maria Mushi mfanyabiashara eneo la CBE amesema uhamasishaji unatakiwa kuanzia katika uongozi wa serikali za mitaa kwani wanaposimama katika nafasi zao kuhamasisha usafi kila mwananchi atakubali ule muitikio.
“Kipindi cha nyuma muhitikio ulikuwa mkubwa kwani viongozi wengi walikuwa mstari wambele katika kuhasisha, hivyo wao wakilegea hata na wananchi unakuta wanalegea katika utendaji,”amesema.
No comments:
Post a Comment