Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye kwa kuisimamia vyema sekta ya mawasiliano na kuwezesha kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini.
Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza hayo leo Mei 13, 2023 jijini Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa minara ya mawasiliano 758 na kuongezea uwezo wa minara 304 ili kuboresha huduma za mawasiliano vijijini.
"Nakupongeza Waziri Nape pamoja na Wizara yako kwa kuandaa tukio hili ,hii ni mara ya kwanza mnafanyakazi nzuri sana katika nchi hii ya kujenga minara 758 kwa mara moja", alieleza Rais Dkt. Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia aliwapongeza wadau wa sekta ya mawasiliano kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini.
Pamoja na hayo Dkt.Samia amewataka watoa vibali vya Ujenzi kuhakikisha vinakamilika ndani ya Mwenzi mmoja ili kutokuwa kikwazo Cha kukamilika Kwa miradi hiyo.
"Hakuna Miezi sita Wala mitatu natoa Mwezi mmoja tu kuhakikisha vibali vyote vya Ujenzi wa minara hii view vikekamilika,"
Na kuongeza kuwa "Niwatake Halmashauri zote kushirikiana na TARURA kuhakikisha njia zinazokwenda maeneo ambayo Minara itajengwa zinapitika,Niwatake pia REA hakikisheni umeme unafika maeneo ya mradi pamoja na changamoto zilizopo ila umeme uende ili kupunguza gharama za uendeshaji,"amesema Dkt.Samia
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alisema kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na wadau ili kusaidia Watanzania kutumia fursa zinazotokana na huduma za mawasiliano ikiwemo za kidigitali.
“Hadi sasa USCAF imeingia makubaliano na kampuni za kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,258 zenye jumla ya vijiji 3,704 na wakazi milioni 15.1, jumla ya minara ya mawasiliano 1,380 itajengwa aidha katika mikataba 19 ambayo UCSAF imeingia na watoa huduma za mawasiliano,”alisema Waziri Nape.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 199.9 na ni ushahidi wa jinsi Serikali inavyothamani na kuhakikisha kuwa watanzania hasa wa vijijini wanapata huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake ,Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa kusainiwa Kwa mikataba hiyo ni ushirikiano uliopo Kati ya Serikali,wadau wa maendeleo na watoa huduma za mawasiliano lengo likiwa ni kukuza mawasiliano hapa nchini hasa maeneo ya Vijijini.
“Hatua hiyo ya ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano 758 na kuongeza nguvu minara ya mawasiliano 304 ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na watoa huduma za mawasiliano”. Alisema Bw. Abdullah.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justine Mashiba amesema katika kutekeleza miradi hiyo, UCSAF ilitangaza zabuni katika maeneo 763 na baada ya mchakato wa zabuni yamepatikana maeneo katika kata 713 ambako minara 758 itakwenda kujengwa Kwa ushiriki wa watoa huduma.
Amewataja watoa huduma ambao watashiriki katika kujenga minara hiyo kuwa ni TTCL ambayo inajenga minara 104 katika kata 104, Vodacom Tanzania itajenga minara katika kata 190 , Airtel Tanzania itajenga minara 168 katika kata 161, MIC Tanzania imeshinda zabuni ya kujenga minara 262 katika kata 244, pamoja na Halotel ambayo imeshinda kata 34 na itajenga minara 34.
“Mbali na kujenga minara hiyo pia tunakwenda kuongeza nguvu minara 304 ambayo ilikuwa inatoa teknolojia ya 2G na sasa itakwenda kutoa teknolojia ya 3G na baadhi ya maeneo itatoa teknolojia ya 4G”. Amesema Bi. Justina.
Ameongeza kuwa katika kuongeza nguvu ya minara hiyo, MIC Tanzania itaongeza nguvu katika minara 148, TTCL minara 55, Airetel minara 32 Vodacom Tanzania minara 69.
Awali Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete, amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yana manufaa kwa watu na maendeleo ya taifa.
“Katika dunia ya sasa uwekezaji wa namna hii unachangia kurahisisha mawasiliano kupitia sauti, video na ujumbe na hasa kwenye elimu, maendeleo ya teknolojia yamechangia wafanyabiashara kupata fursa za kibiashara,”amesema Bw. Belete.
Ameongeza kuwa kwenye maeneo mengi ya Tanzania hasa maeneo ya vijijini wananchi wamekuwa wakiwasiliana kwa sauti bila huduma ya intaneti lakini kupitia mikataba hiyo zaidi ya watanzania milioni tatu watakuwa na uwezo wa kupata intaneti yenye kasi ya juu.
“Benki ya Dunia imekuwa ikisaidia Serikali ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali na katika mradi wa Tanzania ya kidijitali tumetoa dola za Marekani milioni 150”, alisema Bw. Belete.
Aidha, ujenzi wa minara ya mawasiliano itasaidia kuwa na huduma bora ya mawasiliano kwa wananchi wote wa vijijini na taasisi za umma na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni tatu ambao hawakufikiwa na huduma ya intaneti yenye kasi ya 3G.
No comments:
Post a Comment