Bilioni 12.6 kutunza maji ya Victoria Mwanza. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 15, 2023

Bilioni 12.6 kutunza maji ya Victoria Mwanza.


Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kupitia programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM) inatarajia kutumia kiasi cha Euro milioni 5.3, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 12.6 ili kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira jijini Mwanza.
 

Mradi huo utatekelezwa kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza (MWAUWASA) na utahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mitaro yenye urefu wa takribani kilometa 15, ununuzi wa magari ya majitaka na kuunganisha kaya mbalimbali katika mfumo wa majitaka ili kuthibiti tabia ya kutapisha majitaka kutoka katika makazi kuelekea katika ziwa Victoria. 



Naibu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde hilo Mhandisi Coletha Ruhamya ameainisha hayo wakati wa mafunzo maalumu kwa wanahabari jijini Mwanza yakiwahusisha na Maafisa Habari kutoka Wizara Mtambuka ikiwemo Wizara ya Maji.


Amesema programu hiyo ni kubwa na inahitaji ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika jamii ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana wakati wa utekelezaji.


Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Viktoria Dkt. Renatus Shinhu amewashukuru wadau wa maendeleo katika mradi huo ambao ni European Union (EU), Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya KFW pamoja na Serikali ya Tanzania.


Amesema mradi huo utawezesha usalama wa Ziwa Victoria na kuokoa mimea na viumbehai wengine wanaotegemea maji ya ziwa hilo.


Programu ya Pamoja ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya Ziwa Victoria (LVB IWRMP) ni programu ya kikanda inayoratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na kutekelezwa katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment