Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kulinda maslahi ya taifa.
Mkomi alitoa kauli hiyo hivi karibuni, wakati wa kikao kazi cha watumishi wa e-GA na viongozi wa Wizara kilicholenga kujadili utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.
Alisema kuwa, watumishi wa e-GA wanashiriki katika kazi muhimu zinazohusu mifumo na miundombinu muhimu ya TEHAMA serikalini hivyo, wanapaswa kuwa waadilifu kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, pamoja na kutunza siri ili kulinda maslahi ya nchi.
"Nyinyi ndio mnahusika na mifumo ya serikali ikiwemo mifumo nyeti inayohusu rasilimali na usalama wa taifa, hakikisheni nafasi mliyonayo mnaitumia kutekeleza majukumu yenu tu kwa uadilifu na kutunza siri ili kulinda taifa letu", alisema.
Vilevile aliwapongeza watumishi hao kwa weledi na utendaji kazi mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao, hali ambayo inachangia ukuaji wa Serikali Mtandao katika taasisi za umma.
"Napokea simu nyingi sana aidha kutoka kwa Makatibu Wakuu au Wakuu wa taasisi za umma, wakiomba vijana kutoka e-GA hii inaonesha ni jinsi gani mlivyo wazuri katika utendaji kazi wenu" alisisitiza.
Ili kuongeza ufanisi na ubunifu katika TEHAMA, Mkomi aliutaka uongozi wa Mamlaka kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwapa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi.
Alisema, teknolojia hukua na kubadilika kila mara, hivyo ni vema Mamlaka ikaweka utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuweza kukabiliana na mabadiliko hayo.
Kikao kazi hicho kilifanyika katika Ofisi za e-GA zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, na kuongozwa na Mhe. George Simbachawene Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Naibu Waziri Mhe. Ridhiwani Kikwete pamoja na Katibu Mkuu Bw. Juma Mkomi.
No comments:
Post a Comment