Na Mwandishi Wetu - Singida
Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Singida, Mhandisi Claver Mwinuka ameongoza watumishi wa Wakala mkoani humo kushiriki katika bonanza maalum la michezo lililolenga kujenga na kuimarisha afya pamoja na kuongeza mshikamano miongoni mwao.
Bonanza hilo lililofanyika katika uwanja wa Bombadia mkoani Singida limewakutanisha watumishi wa TARURA pamoja na taasisi nyingine zikiwemo Shiriki la Nyumba la Taifa, TANROADS na Mahakama ambapo lilipambwa na michezo ya kuvutia ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio za magunia, kukimbiza kuku, mchezo wa bao pamoja na mpira wa pete.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mhandisi Mwinuka amezishukuru taasisi zilizojumuika na Wakala katika bonanza hilo huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora na kuimarisha mahusiano kazini. “Michezo ni njia mojawapo ya kuimarisha afya ya mwili na akili, lakini pia huchangia katika kujenga mshikamano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja kama timu,” amesema.
Pia amewahimiza watumishi kuwa na utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kuendelea kushiriki michezo kazini ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha afya zao.
Naye, Meneja wa Shiriki la Nyumba la Taifa Mkoa wa Singida, Bi. Judith Mwalongo ameipongeza TARURA kwa kuandaa michezo hiyo inayolenga kuburudisha na kuimarisha mahusiano ya kikazi na amewahimiza watumishi kushirikiana katika maeneo ya kazi.
"Tukitaka kufanikiwa katika kufikia malengo yetu, suala la ushirikiano ni lazima liwepo kati yetu, tutumie michezo na mazoezi kama nyenzo ya kujenga ushirikiano baina yetu"
Bonanza hilo limeonesha kuwa, mbali na majukumu ya kikazi, TARURA inatambua umuhimu wa shughuli za kijamii na kiafya kwa ustawi wa watumishi wake, hali inayoonyesha umuhimu wa michezo katika kuleta umoja na kuimarisha afya za wafanyakazi.














No comments:
Post a Comment