
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imesema kufuatia utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Migodi nchini imenunua bidhaa na huduma kutoka kampuni za Watanzania zenye thamani ya shilingi trilioni 3.8 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma Machi 16, 2026 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Amesema bidhaa na huduma 20 zimetengwa mahsusi kwa kampuni zenye umiliki wa asilimia 100 ya Watanzania, zikiwemo kampuni zinazomilikiwa au kuajiri vijana, hatua iliyochangia kuongeza ushiriki wa wazawa katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamando amesema Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya madini katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwemo kutenga maeneo zaidi ya uchimbaji kwa vijana katika mikoa mbalimbali kulingana na aina ya madini yanayopatikana.
Amesema pia Tume itaendelea kuandaa minada na maonesho ya madini ya vito pamoja na kuhamasisha vijana kushiriki katika zabuni mbalimbali zitakazotangazwa wakati wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Aidha, Tume ya Madini inaendelea kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia na kuwajengea vijana ujuzi wa matumizi ya vifaa vya kisasa katika utafutaji na uchimbaji wa madini.
Kamando ameongeza kuwa Tume imeingia makubaliano na Benki ya CRDB yaliyosainiwa Februari 23, 2026 yatakayowezesha wachimbaji wadogo wa dhahabu, hususan vijana, kupata mitaji ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Kuhusu uongezaji thamani wa madini, amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kusimamia sera na sheria zinazohakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Ameeleza kuwa hadi sasa kuna viwanda saba vya kusafisha madini vinavyofanya kazi nchini na sekta hiyo imezalisha ajira 273, nyingi zikinufaisha vijana, huku madini yenye thamani ya shilingi trilioni 5.802 yakiongezewa thamani ndani ya nchi kati ya Julai na Desemba 2025.
Pia kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (Mining for Better Tomorrow – MBT), Tume ya Madini imetoa leseni 273 kwa vikundi 183 vya vijana kati ya Julai na Desemba 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera, Shinyanga, Morogoro, Dodoma na Njombe.
Vikundi hivyo vinajihusisha na uchimbaji wa dhahabu, shaba, madini ya vito, chumvi na madini ya ujenzi, ambapo hadi Desemba 2025 vijana 2,550 walikuwa wamepata ajira za moja kwa moja kupitia mradi huo.
Kamando ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwa kutoa leseni 5,983 kati ya Julai hadi Desemba 2025, sawa na asilimia 71 ya leseni zote zilizotolewa katika kipindi hicho, huku sehemu kubwa ya waombaji wakiwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45.
Kwa upande wa maeneo ya uchimbaji, amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imependekeza kutenga maeneo 65 maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika mikoa ikiwemo Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Geita, Shinyanga, Mwanza na Mbeya.






No comments:
Post a Comment