Naibu Waziri Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe, amesema Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilikokuwa zikivikabili vyama vya ushirika nchini.
Mhe.Kigae alitoa kauli hiyo juzi, wakati wa uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane Ipuli Mkoani Tabora.
Alisema, kumekuwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa vyama vya ushirika kwa muda mrefu ikiwemo wakulima kudhulimiwa mazao yao hali iliyopelekea baadhi ya wakulima kuijiondoa katika vyama hivyo, lakini kupitia mfumo wa MUVU mkulima ataepukana na tatizo hilo.
‘’Hapo mwanzo kulikuwa na changamoto kubwa kwenye hivi vyama vya ushirika,mpaka ilifikia hatua wakulima wakakasirika na wengine kujiondoa kwenye vyama, sasa huu Mfumo umeleta maboresho makubwa yatakayosaidia mkulima kutokupunjwa mazao yake’’, alisema.
Meneja wa TEHAMA Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika (TCDC), Hermes Sotter alisema, Mfumo wa MUVU umeongeza uwazi katika uendeshaji wa vyama vya ushirika kwakuwa umeunganishwa na Mfumo wa Mizani ya Kidigitali unaomuwezesha Mkulima kupokea taarifa za mzigo wake ikiwemo risiti na ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya mkononi, mara baada ya kupimiwa kwenye chama cha ushirika.
Nao wakulima kutoka katika vyama mbalimbali vya Ushirika, wameeleza kuridhishwa na mfumo huo kwakuwa hivi sasa wanapata taarifa zote kuhusu mazao yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali hivyo hawana wasiwasi tena kwani kila kitu kinapitia kwenye Mfumo.
Mfumo wa MUVU umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika-TCDC kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili sekta ya ushirika.
No comments:
Post a Comment