Na Mwandishi wetu -Dar Es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo tarehe 24, Juni 2023 imetekeleza wajibu wake kwa jamii kwa kufanya usafi katika Soko la Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam.
Katika kutekeleza zoezi hilo BRELA imetoa vifaa mbalimbali vya usafi na kuungana na wafanyabiashara wa soko hilo kufanya usafi.
Akitoa salam za Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Afisa Utumishi, Bi. Lydia Rimoy ametoa wito kwa uongozi wa soko la Buguruni kuwahimiza wafanyabiashara kurasimisha biashara zao ili waweze kutambulika.
“Ni muhimu sana kwa kila mfanyabiashara katika soko hili kurasimisha biashara yake. Kuna faida nyingi zinazoambatana na urasimishaji huo, ikiwa ni pamoja na kutambulika na taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo, kuaminika na wateja, kutii matakwa ya kisheria, kutangaza biashara na nyingine nyingi”, amesema Bi. Rimoy.
Ameongeza kuwa BRELA imetoa vifaa hivyo vya usafi kwa kuzingatia kuwa wafanyabiashara ndiyo wadau wake wakubwa hivyo ni vyema mazingira wanayofanyia biashara zao yawe rafiki.
“Tumefika hapa kushiriki nanyi zoezi la usafi katika soko hili ambapo ndani yake wapo wafanyabiashara ambao wanatakiwa kuwa na Leseni za Biashara kundi “A” na wengine wanatakiwa kusajili Kampuni au hata Majina ya Biashara na huduma zingine kutoka BRELA, hivyo nyie ni wadau wetu wakubwa”, Amesema Bi Rimoy.
Pia amesitiza kuwa BRELA itaendelea kushirikiana na uongozi wa soko hilo ili kuweka mpango mkakati wa kuwasogezea huduma za papo kwa papo itakapohitajika ili wapate fursa ya kurasimisha biashara wakiwa katika maeneo yao.
Naye Msimamizi wa Wafanyakazi na Mkuu wa Takwimu wa Soko la Buguruni Bw. Reuben Shiyo ameupongeza uongozi wa BRELA kwa kutekeleza zoezi la kurejesha kwa jamii ikiwa ni pamoja na kufanya zoezi la usafi kwa vitendo.
Zoezi hilo limekuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo hufanyika kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23 chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa Mwaka 2023 Maadhimisho hayo yaliongozwa na kauli mbiu “Uhusiano kati ya Uwezeshaji wa Vijana na Usimamizi wa masuala ya Uhamiaji: Kujenga Utamaduni wa Utawala Bora, Matumizi ya TEHAMA na
Ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi.”
No comments:
Post a Comment