DKT.MPANGO AAGIZA UBORESHAJI MICHEZO MASHULENI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 6, 2023

DKT.MPANGO AAGIZA UBORESHAJI MICHEZO MASHULENI


Na Angela Msimbira, TABORA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameziagiza wizara za kisekta kuhakikisha shule za msingi na sekondari inakuwa na mwalimu wa michezo ili kuboresha michezo nchini.


Wizara hizo ni Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.


Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo Juni 6, 2023 wakati wa kufungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa shule za Sekondari (UMISSETA) uliofanyika mkoani Tabora.



Amesema uwepo wa mwalimu wa michezo shuleni kutasaidia uimarishaji wa michezo, kuwawezesha watoto kufundushwa michezo kitaalam na kufundishwa bila kukosa.


Dkt. Mpango amewaagiza wasimamizi wa elimu nchini kuhakikisha wanalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo na kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya shule mpya unaenda sambamba na uwepo wa viwanja vya kutosha vya michezo.


“Kumekuwa na baadhi ya maeneo kubadili matumizi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya viwanja vya michezo na kkujenga madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo suala hili halikubaliki, hakikisheni maeneo hayo yanalindwa.”


Dkt. Mpango pia amewataka kuhakikisha uboreshaji wa miundombinu ya shule uende sambamba na usafi wa mazingira kwa kusimamia upandaji wa miti kuzunguka viwanja vya michezo ili vijana wanapocheza wanapata hewa safi na kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia michezo


Pia amesisitiza umihimu wa kufuata ratiba za michezo mashuleni na kuonya vikali tabia ya baadhi ya shule kutokutenga muda wa michezo kwa kuwa ni wajibu wanafunzi wakapata muda wa kuzingatia michezo baada ya masomo ili kuibua na kuendeleza vipawa vyao,amewataka wasimamizi wa elimu nchini kusimamia suala hili.


Dkt. Mpango pia ameziagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuweka mikakati ya kuboresha michezo kwenye shule za serikali kwa kuwa na maeneo ya kutolea mafunzo stahiki kwa watoto (academy za michezo).

No comments:

Post a Comment