CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA MIUNDOMBINU INAENDELEA KUJENGWA KILA KONA YA NCHI - ULEGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 13, 2026

CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA MIUNDOMBINU INAENDELEA KUJENGWA KILA KONA YA NCHI - ULEGA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya miundombinu nchini, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya kuijenga na kuikuza Tanzania.

Ulega ameyasema hayo mkoani Tanga alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 pamoja na barabara ya Tanga – Pangani yenye urefu wa kilometa 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Akifafanua kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Ulega amesema utekelezaji wake ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kuimarisha maendeleo ya wananchi.

“Mhe. Mwenyekiti, kila mahala katika nchi hii panajengwa. Hatua hii inaonesha uimara na kasi ya maendeleo ya nchi yetu kupitia Sekta ya Ujenzi yanayotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Ulega.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Joyce Ndalichako, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuijenga na kuiunganisha nchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu.

Amesema miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa madaraja, barabara za lami na viwanja vya ndege ina mchango mkubwa katika kufungua fursa za kiuchumi, kurahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea maendeleo ya Taifa.


No comments:

Post a Comment