* Iko kwenye nchi karibu 50 duniani, ikiwemo nchi 10 za Afrika
* Inaendesha bandari kwenye mataifa makubwa duniani, ikiwemo Marekani, China, Ujerumani, Ufaransa na Canada
* Kwa Afrika, wapo Nigeria, Afrika Kusini, Rwanda, Misri, Msumbiji na nchi nyingine
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Tanzania inatarajia kuingia makubaliano na kampuni ya Dubai ya DP World ya kuweka uwekezaji binafsi kwenye bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi na kiwango cha mizigo inayopita kwenye bandari hiyo.
DP World ni moja ya kampuni kubwa duniani zenye mafanikio katika uendeshaji wa bandari katika nchi mbalimbali.
Kwa mwaka 2022 peke yake, DP World ilipata mapato ya Dola za Marekani Bilioni 17.1 na faida ya Dola Bilioni 5 (sawa na shilingi trilioni 12).
Kwa upande wa Afrika, DP World inafanya kazi kwenye nchi za Algeria, Angola, Djibouti, Misri, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal, Somaliland na Afrika Kusini.
DP World imewekeza zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 1.8 kwenye bara la Afrika katika miaka kumi iliyopita na inapanga kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 3 (shilingi trilioni 7.2) kwenye bara hili katika miaka ijayo.
Serikali ya Tanzania inatarajia kusaini makubaliano na Serikali ya Umoja wa Falme.za Kiarabu (Dubai) wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania.
Mkataba huo unakuja baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of
Understanding - MOU) na Kampuni ya DP World mwaka jana.
Uwekezaji binafsi kwenye Bandari ya Dar es Salaam siyo jambo geni.
Kampuni binafsi ya TICTS imeendesha eneo la makontena la bandari hiyo kwa zaidi ya miaka 30 hadi mwaka jana ambapo Serikali ya Tanzania iliamua kutoendeleza mkataba huo ili itafute mwekezaji mwingine wa nje wa kimkakati.
Chini ya TICTS, eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam lilikuwa likilalamikiwa sana kutokana ufanisi duni.
Bandari ya Dar es salaam ni lango la kuu la kibiashara la Tanzania. Takribani asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na Bandari hii.
Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Ujio wa DP World unatarajiwa kuongeza ufanisi kwenye bandari ya Dar es Salaam na kuleta mzigo mkubwa ambao utaongeza mapato ya serikali.
Bandari ya Dar es Salaam iko kwenye ushindani mkubwa na bandari nyingine za bara la Afrika, ikiwemo bandari za nchi za Afrika Kusini, Msumbiji na Namibia.
Bandari ya Dar es Salaam inatarajia kuhudimia shehena ya mizigo ya tani milioni 20 kwa mwaka 2022/23, huku bandari ya Durban ya Afrika Kusini ikiwa inahudumia shehena za mizigo ya zaidi ya tani milioni 31 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment