SERIKALI YATIA SAINI MKATABA TATHIMINI YA MAZINGIRA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 6, 2023

SERIKALI YATIA SAINI MKATABA TATHIMINI YA MAZINGIRA.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz (kushoto) wakikabidhiana Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa masuala ya Mazingira (TANSEQ) Bwa. Lusako Raphael (kulia) baada ya utiaji saini hafla iliyofanyika Juni 06, 2023 katika Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz akitia saini Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) wakati wa hafla hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) iliyofanyika Juni 06, 2023 katika Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa masuala ya Mazingira (TANSEQ) Bwa. Lusako Raphael akitia saini Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) wakati wa hafla hiyo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)


Na; Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali imetia saini Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP).


Akizungumza mara baada ya kutia saini mkataba huo Juni 6, 2023 Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonaz amesema mkataba huo ,utawezesha kufanyika kwa tathmini ya athari ya mazingira pamoja na matengenezo ya meli zitakazotumika katika uvuvi wa Bahari Kuu ili kupata mazao ya bahari yatakayochangia katika uchumi wa Nchi.


Dkt. Yonaz aliendelea kusema kuwa, sambamba na tathmini hiyo pia utafanyika upembuzi yakinifu katika kuundwa kwa vyombo hivyo kazi itakayofanyika kwa muda wa siku 75 ambapo itagharimu shilingi milioni 349 huku akisisitiza umakini katika usimamizi wa utekelezaji wa kazi hiyo.


“Tanzania inazo rasilimali nyingi za majini, sasa ili kuhakikisha tunainua uchumi kupitia Uchumi wa Bluu Serikali imeona ni muhimu kutengeneza meli kubwa zitakazovua katika kina kirefu ili kupata mazao ya bahari ambapo meli nne zitatengenezwa kwa ajili ya Zanzibar na Meli tano kwa Tanzania Bara hivyo kukamilika kwake kutasaidia kuinua uchumi wa Taifa." Amesema Dkt. Yonazi.


Pia Katibu Mkuu huyo amewahimiza wadau wa uvuvi ambao ni Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) kushirikian ana Mkandarasi huyo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kikamilifu huku akihimiza kila mmoja kuwajibika kwa sehemu yake kwa lengo la kupata matokeo chanya.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa masuala ya Mazingira (TANSEQ) Bw. Lusako Raphael amebainisha kwamba lengo la kufanya tathimini hiyo ni kuhakikisha mradi hausababishi athari hasi katika mazingira na jamii.


“Mradi huu unalenga kuwezesha ununuzi wa meli pamoja na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata samaki hivyo tunategemea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote kama ZAFICO, TAFICO na Wizara ya Kilimo. Pia kuna mkakati wa kudhibiti athari za mazingira ambao ndiyo utakuwa muongozo wa utekelezaji wa mradi.' Ameeleza Mkurugenzi huyo.


Ikumbukwe kuwa AFDP ni mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).

No comments:

Post a Comment