Mabingwa watetezi wa mpira wa Wavu wasichaa Mkoa wa Mtwara, wamefanikiwa kuingia fainali kwenye Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yanayoendelea Mkoani Tabora.
Mkoa wa Mtwara ambao ni mabingwa mara tisa mfulululizo wa UMITASHUMTA, wameingia fainali baada ya kushinda seti 3-0 dhidi ya Katavi katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa leo Tarehe 11 Juni 2023, kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Tabora majira ya Saa 2 Asubuhi.
Kocha wa Timu ya Mtwara ambayo inawania kuweka historia ya kushinda Ubingwa wa UMITASHUMTA kwa mara ya 10 mfululizo Gabriel Joshua, amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo akisema sasa wanaangalia zaidi mchezo wa fainali ambao watakutana na Mkoa wa Manyara.
“Vijana wamecheza vizuri, wanajiamini na wanafuata maelekezo wanayopewa ndio maana unaona hata uchezaji wao ni tofauti katika kila mchezo walioingia viwanjani, washindani wetu tuliokutana nao kwenye michezo hii ukiwauliza watakuambia utofauti wetu na wao” amesema Mwl. Joshua
Katika nusu fainali nyingine ya Wavu iliyochezwa kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Tabora Wavulana, Mkoa wa Manyara ulifanikiwa kuingia fainali baada ya kuwashinda Lindi kwa Seti 3-2 katika mchezo wa kuvutia.
Kwa matokeo hayo sasa Mtwara itakutana na Manyara kwenye fainali ya Wavu Wasichana, katika Mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumatatu Tarehe 12 Juni 2023, huku Lindi na Katavi wakikutana kumtafuta atakayeshika nafasi ya tatu.
No comments:
Post a Comment