OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUENDELEA KUWANOA WABUNGE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 8, 2023

OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUENDELEA KUWANOA WABUNGE


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Ofisi hiyo itaendelea kutoa semina kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi uhusu tafsiri na dhana halisi kuhusu manufaa na faida za Biashara ya Kaboni ili kujenga uelewa wa pamoja katika jamii.


Akizungumza Juni 07, 2023 jijini Dodoma wakati wa kufunga semina kwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Maji na Mazingira, Naibu Waziri Khamis amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha elimu kuhusu Biashara ya Kaboni inawafikia wabunge ambao wana ushawishi mkubwa kwa wananchi.


“Tumekusudia kutoa mafunzo haya kwa wabunge na wajumbe wa kamati zetu, mafunzo haya yanakuwa endelevu kwani sisi wabunge tuna ushawishi mkubwa katika jamii na tunalosema tunasikilizwa na wananchi” amesema Khamis.


Aidha Mhe. Khamis amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka maswali kutoka kwa wabunge na wananchi kwa ujumla kuhusu tafsiri na dhana halisi ya biashara hii huku wabunge wengi walipenda suala hili lipatiwe ufafanuzi wa Serikali kuhusu biashara ya kaboni, hivyo kwa kutambua umuhimu huo serikali imeandaa mpango wa mafunzo na semina mbalimbali kwa wabunge.


Pia, amewataka wabunge kuwa mstari wa mbele katika suala zima la uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiwemo kuhamasisha jamii katika shughuli za upandaji wa miti, utunzaji wa vyanzo vya maji kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha kuunga mkono juhudi za serikali katika kusukuma mbele ajenda ya mazingira.


Awali akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. Jackson Kiswaga ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa semina hiyo na kutoa wito kwa kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanakuwa endelevu ili kuweza kuwajengea uwezo wabunge.


“Katika hili la Biashara ya Kaboni, naipongeza Serikali kwa hatua hii muhimu tuliyofikia ambayo imelinda zaidi maslahi ya taifa kuhusu rasilimali za misitu. Hapa kwetu square metre moja ni takribani dola 80 ikilinganisha na Marekani ambapo ni Dola 50 kwa square metre moja, hivyo ni jambo la kujipongeza na tunapaswa kuweza mikakati madhubuti ili tuweze kunufaika” amesema Mhe. Kiswaga


Aidha, Kiswaga ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais kuweka utaratibu wa usimamizi mahsusi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaozungukwa na rasilimali zitokanazo na Biashara ya Kaboni ikiwemo misitu wananufaika kupitia miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi itakayoibuliwa na wawekezaji.


Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imejipanga kukamilisha utekelezaji wa miradi yote ya mazingira iliyopo pande zote za Muungano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kunufaika na hivyo kufikia malengo ya miradi hiyo.


“Hivi karibuni tumepata ‘extension’ (kuongezewa muda) katika miradi ya mazingira, hivyo tumejipanga kuhakikisha kuwa miradi yote iliyopo upande wa Tanzania Bara na Zanzibar inakamilika kama ilivyopangwa” amesema Bw. Mitawi.


Katika semina hiyo ya siku moja wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais waliwasilisha mada mbalimbali ikiwemo wasilisho kuhusu Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, wasilisho kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na wasilisho kuhusu masuala ya Muungano.

No comments:

Post a Comment