Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiongea na kutatua changamoto za wafanyabiashara wa jiji la Dodoma katika ukumbi wa Jiji jana tarehe 08/06/2023 Mkoa wa Dodoma. |
Na Mwandishi wetu -Dodoma
Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amekutana na wafanyabiashara wa Mkoa wake kwa lengo la kujadili changamoto za biashara kwa ujumla na kuweka maazimio yenye tija katika kukuza masoko kwa kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi.
Kikao hicho kimefanyika Juni 8, 2023 katika Ukumbi wa jiji Mkoani humo na kuhudhuriwa na wafanyabiashara wakubwa, wakati na wadogo wakiwemo viongozi wa masoko, wamiliki wa shule, wamiliki wa Nyumba za wageni, Viongozi wa makampuni mbalimbali, wauza vipodozi na wafanyabiashara wa Mbao. Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Taasisi za Serikali ikiwa ni pamoja na TANROADS, TRA, OSHA, TBS, LATRA, BRELA na Tanzania Commercial Bank (TCB).
Awali wafanyabiashara walifanikiwa kutoa changamoto mbalimbali zinazowakabili ndani ya masoko zikiwemo ulipishwaji wa kodi ya pango ikiwa siyo wamiliki wa nyumba, wingi wa kodi kwa wafanyabiashara, ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara, upungufu katika kaguzi za risiti, mfumo wa ulipaji kodi usio rafiki na changamoto za uzoaji wa taka na maji taka.
"Sisi Mkoa wa Dodoma tuna dhamira ya kuhakikisha wafanyabiashara wanakaa katika Mazingira mazuri na tunajipanga kufanyia kazi changamoto na maazimio ili kuendelea kuboresha huduma katika nyanja zote "amesema Senyamule
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa huyo ametoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa Serikali na kuwahakikisha uwepo wa Mazingira rafiki ya biashara ikiwa ni utekelezaji wa agizo na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amewataka kuunda umoja kulingana na biashara wanazofanya ili iwe rahisi kuratibu hoja zinazojitokeza na kuziwasilisha Serikalini.
Nae, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu amewapongeza wafanyabiashara kwa kujumuika pamoja katika kuwasilisha changamoto zilizopo ndani ya masoko na kuweka kwa pamoja mikakati ya ufumbuzi na amewasisitiza kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu.
"Serikali itahakikisha eneo letu la Makao Makuu ni sehemu sahihi na wezeshi kwa wafanyabiashara, lazima kuwa na mahali sahihi pakufanya biashara eneo ambalo halitakuwa na changamoto ili biashara ziweze kushamiri na kuweza kupata faida ninyi kwa mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla" Amesema Gugu
Kikao hicho, kiliazimia maazimio ambayo yataboresha biashara zao ikiwa ni pamoja na Halmashauri kuchukua hatua madhubuti kwa wanaomiliki vizimba na kutofanya biashara, kuundwa kwa timu itakayopitia Sheria ya kodi ili kuunganisha Serikali na sekta binafsi na kuundwa kwa kamati ya utatuzi wa changamoto za masoko kama ilivyokuwa kwa soko la Machinga.
Maazimio mengine yaliyokubalika ni pamoja na kuwepo kwa taasisi moja ya kukusanya tozo, Jiji kukamilisha miundombinu kwenye baadhi ya masoko na kutoa elimu kwa umma hususan wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mfumo wa TAUSI.
No comments:
Post a Comment