Na Angela Msimbira, Tabora
Michuano ya UMITASHUMTA inaendelea kupamba moto katika viwanja mbalimbali mkoani Tabora baada ya timu za michezo mbalimbali kuoneshana kazi.
Katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, timu ya netiboli ya Mkoa wa Morogoro imeicharaza timu ya Kilimanjaro baada ya kukubali kipigo cha magoli 22- 16.
Pia timu ya Shinyanga imetoka hoi baada ya kukubali kichapo cha magoli 28-14 dhidi ya timu ya Kigoma huku wenyeji wa michuano hiyo timu ya Tabora imeibuka kidedea dhidi ya Unguja kwa magoli 32-9.
Timu ya Simiyu imehenyeshana na timu ya Mara kwa magoli 28- 24 wakati timu kutoka makao makuu ya nchi ya Dodoma ikiiadhibu Kagera magoli 34- 25 huku timu ya Dar es Salaa ikiinyuka Manyara kwa magoli 23-22
Kwa upande wa mpira wa soka wasichana, timu ya Ruvuma imepata kibano kutoka Mwanza kwa kufungwa mabao 11-0 huku Iringa iikinyukwa na Singida mabao 8-0 wakati Mara ikitoa dozi kwa Songwe kwa mabao 8-0.
Timu ya Dar-es Salaam imeitambia Mtwara kwa mabao 6-0, huku Geita ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Arusha wakati Pwani ikitoka uwanjani ikiwa imelowa baada ya kupokea kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Tanga.
Kwa upande wa mpira wa kikapu wasichana, Mkoa wa Singida imeifunga Kagera kwa pointi 7-3, wakati Mkoa wa Arusha iliichabanga Songwe kwa pointi 32-2 na Shinyanga kuibuka na ushindi wa pointi 26 – 10 dhidi ya Mwanza.
Aidha, kwa upande wa mpira wa kikapu wavulana Dar es salaam imeifunga Pemba kwa pointi 22-19, timu ya Shinyanga imeibuka kidedea kwa kuifunga Kigoma kwa pointi 14- 04 huku wenyeji Tabora wakiilaza Dodoma kwa pointi 23-11 na Mkoa wa Mwanza ikiipiga Tanga kwa pointi 29-24
No comments:
Post a Comment