Na. Lusungu Helela-Dodoma
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa rai kwa Taasisi Simamizi na Vyama vya Kitaaluma kuhimiza na kuwasimamia watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha Watalaamu Waandamizi wa Taasisi Simamizi na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.
Bi. Shuli amesema kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi katika sekta ya afya, manunuzi, ujenzi pamoja na elimu ambayo yanahusu uvunjifu wa maadili, hivyo anaamini mafunzo hayo waliyoyapata kwa muda wa siku mbili yatasaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Bi. Shuli amezitaka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma kujenga imani kwa wananchi na kuonesha thamani ya fedha zinazowekezwa na serikali katika miradi mbalimbali kwa kuwasimamia ipasavyo wataalamu wao katika utendaji kazi wao wa kila siku
‘’Ni matarajio yetu kupitia mafunzo haya tutakuwa na utumishi uliotukuka kwa kuwa na Watumishi wa Umma wenye kuzingatia weledi na wachapa kazi ili kuendelea kulinda taswira nzuri ya serikali ’’ amesema Mwakilishi wa Katibu Mkuu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Madilli kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika amesema kikao kazi hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja ya usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma pamoja na kujadili mikakati mbalimbali itakayowasaidia kusimamia suala la maadili kwa watumishi wa umma.
"Katika kuhakikisha suala hili linakuwa endelevu tumeweka mikakati ya pamoja kwa lengo la kuhakikisha suala la maadili katika utumishi wa umma linasimamiwa ipasavyo" amesisitiza Bi. Mavika.
Naye Afisa Muuguzi kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Rehema Msanjila amesema mafunzo aliyoyapata yataenda kuleta mapinduzi makubwa katika eneo analolifanyika kazi ikizingatiwa sekta ya afya imekuwa ikilalamikiwa sana katika uvunjifu wa maadili.
“Nina imani kubwa kutokana na mikakati mikubwa tuliyojiwekea katika kikao hiki, tunakwenda kuwa na wauguzi na madaktari wenye kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali zetu hapa nchini’ amesema Bi. Msanjila.
No comments:
Post a Comment