THBUB YATOA WITO KWA SERIKALI KUHAKIKISHA SUALA LA KUTOKOMEZA AJIRA KWA WATOTO LINAPEWA KIPAUMBELE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 12, 2023

THBUB YATOA WITO KWA SERIKALI KUHAKIKISHA SUALA LA KUTOKOMEZA AJIRA KWA WATOTO LINAPEWA KIPAUMBELE

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Khamis Hamad akitoa Tamko la THBUB kuhusu ajira kwa watoto Makao Makuu ya Ofisi za Tume Kilimani, jijini Dodoma leo Juni 12, 2023.
Baadhi ya viongozi wa THBUB na waandishi wa habari wakimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Tume (hayupo pichani) wakati akitoa Tamko la Tume kuhusu ajira kwa watoto Makao Makuu ya Ofisi za Tume Kilimani, jijini Dodoma leo Juni 12, 2023.


Na Okuly Julius-Dodoma

Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa wito kwa Serikali kuendelea kuhakikisha suala la kutokomeza tatizo la ajira kwa watoto linapewa kipaumbele katika utengenezaji wa sera, shughuli za kitaifa na kimataifa, katika ushirikiano wa maendeleo na katika mikataba ya kifedha, biashara na uwekezaji;


Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohamed Khamis Hamad wakati akitoa tamko la THBUB katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ajira kwa Watoto leo Makao Makuu ya Ofisi za Tume Kilimani, jijini Dodoma Juni 12, 2023.


Ambapo Muhamed amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kutoa elimu ya haki za mtoto na madhara ya ajira mbaya kwa watoto;


Pia ,jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wote wanaowaajiri na kuwatumikisha watoto; na Wazazi na walezi wahakikishe wanawatunza, kuwalinda na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi. Aidha, wahakikishe watoto wote wanahudhuria shule na hawawatumii kama vitega uchumi vya familia kwa kuwafanyisha kazi ngumu zisizofaa na zinazowaathiri.


"Tunapoadhimisha siku hii, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau mbalimbali wa haki za mtoto duniani katika kupinga ajira kwa watoto, sambamba na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ajira hizo kupitia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: “Haki ya Jamii kwa Wote. Kukomesha Ajira ya Watoto!"


Na kyongeza kuwa "tume inatambua na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kutokomeza ajira kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuridhia Mikataba ya Kikanda na Kimataifa, kutunga Sera na Sheria ya Mtoto ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar ambapo zinakataza mtoto kuhusishwa katika kazi yoyote itakayoweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake,"amesema Muhamed


Ameongeza kuwa ,pamoja na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa, bado zipo changamoto kadhaa, ikiwemo watoto kuendelea kufanyishwa kazi ngumu katika maeneo ya kazi za ndani, mashambani, mitaani, na migodini. Ajira hizi zimekuwa kichocheo cha ukatili dhidi ya watoto ambapo baadhi yao hukosa masomo, kunyonywa kiuchumi kwa kuwa hulipwa ujira mdogo na matatizo ya kiafya, jambo linaloathiri ukuaji wao.


Miongoni mwa sababu zinazoendelea kuchangia ajira kwa watoto ni pamoja na umasikini na jamii kukosa uelewa juu ya madhara ya ajira hizo, hali inayopelekea watoto kufanya kazi ngumu ili kujikimu.


Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, THBUB inaendelea kuhamasisha jamii kuheshimu haki za binadamu katika masuala ya kazi na ajira, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria, Sera na Miongozo mbalimbali inayolinda haki za mtoto nchini. Pia, THBUB inatoa wito kwa Serikali, wadau na jamii kuunganisha nguvu kupinga ajira kwa watoto mahali popote nchini.


‘Haki ya Jamii kwa Wote. Kukomesha Ajira ya Watoto!’


No comments:

Post a Comment