Walimu darasa la awali wajengewa uwezo - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 20, 2023

Walimu darasa la awali wajengewa uwezo

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt.Aneth Komba akifungua mafunzo ya darasa la Elimu ya Awali jijini Dodoma.

Na Joyce Kasiki,Dodoma


MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt.Aneth Komba amewataka walimu na wadhibiti Ubora wa shule kuhakikisha vitabu vyote vikiwemo vya darasa la elimu ya awali vinavyotumika shuleni ni vile vilivyopata ithibati tu na siyo vinginevyo.


Dkt.Komba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa walimu wa darasa la awali yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire (CiC) kupitia Mradi wake wa Watoto Wetu Tunu Yetu uanaotekelezwa katika mikoa ya Dodoma,Morogoro na Mwanza kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Kwa mujibu wa kiongozi huyo matumizi ya vitabu vilivyopata Ithibati yatasaidia watoto kujifunza yale yaliyoandaliwa kwa ajili yao hasa watoto wadogo ambao ndiyo wanaanza kujifunza vitu ikiwemo maadili ya kitanzania.


“Serikali inasisitiza matumizi sahihi ya vitabu vya ziada na kiada ambavyo vina ithibati,kuna utaratibu wa vitabu kupewa ithibati na Kamishna wa Elimu,kwa hiyo wanafunzi watumie vitabu ambavyo vimeidhinishwa na serikali ,na ili tuhakikishe kwamba tunapenda utamaduni wa kujisomea ni muhimu mtoto atumie vitabu vyote vya kiada na ziada.”amesema Dkt.Komba


Katika hatua nyingine amewaelekeza Wadhibiti Ubora wa shule wakasimamie vyema utekelezaji wa mafunzo hayo ili kuhakikisha kwamba baada ya mafunzo hayo walimu wanakwenda kutumia mafunzo hayo kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wa darasa la awali.


“Mnapaswa mkakague na kuhakikisha kweli mwalimu anaandaa darasa changamshi ,anaandaa zana za kutosha za kufundishia na watoto wanaweza kupata ule umahiri uliokusudiwa hasa mahiri za Kusoma,Kuandika na Kuhesabu.”amesema na kuongeza kuwa


Kwa upande wake mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu unaolenga kuimarisha elimu ya darasa la awali Lustica Turuka amesema,ni matumaini ya mkoa wa Dodoma kwamba mafunzo hayo yanakwenda kuwapatia walimu mbinu mpya za ufundishaji wa darasa la elimu ya awali.


“Lakini pia tunategemea ,walimu hawa watakuwa walimu wa mfano kwa ajili ya shule nyingine ambazo walimu wake hawajapata mafunzo haya kwa sababu tumetoa mwalimu mmoja kwenye kila kata ,hii inamaanisha kwamba yule mwalimu aliyepata mafunzo haya ,anakwenda kuwaambukiza wenzake ambao hawajapata mafunzo haya.”amesema na kuongeza kuwa


“Hatutaki tena ule utaratibu wa kufundishia watoto wa darasa la awali chini ya miti ,tunataka kuona wanafunzi wa daras la elimu ya awali wanasoma kwenye madarasa mazuri na ambayo ni changamshi na yanayoongea ambayo humwezesha mtoto kujifunza kwa kuona na kucheza lakini pia kupenda shule na mwisho wa siku tunategemea mafanikio makubwa sana hasa kwenye suala la kusoma,kuandika na kuhesabu kwa sababu darasa la elimu ya awali ndiyo msingi wa madarasa mengine yote.”


Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa CiC Heri Ayubu amesema kuwa mradi huo wa "Watoto Wetu Tunu Yetu" unatekelezwa katika mikoa mitatu ya Mwanza, Morogoro na Dodoma ukiwa na lengo la kuendelea kuchangia uboreshaji wa utoaji wa elimu ya Awali nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali.


Amesema kuwa,mwisho wa mradi huo wanatarajia kuona ongezeko kubwa la wanafunzi wenye utayari wa kuingia darasa la Kwanza kwa kuweza kumudu KKK kwa maana ya Kusoma,Kuandika na Kuhesabu. 


Mwalimu Kinara wa darasa la awali kutoka wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ambaye alishapata mafunzo hayo kupitia Mradi huo wa Watoto Wetu Yetu ulioanza kutekelezwa wilayani humo mwaka 2019 Regina Masawe amesema,mafunzo hayo yamemwezesha kupata nyanja nyingi za ufundishaji wa watoto wa darasa la awali na ufundishaji wake ulikuwa ni tofauti na wakati hajapata mafunzo.


Naye mwalimu wa shule ya Msingi Igoji Kaskazini Wilayani Mpwapwa Frank Masamale amesema,amefurahishwa na CiC kutambua umuhimu wa elimu ya awali na kuandaa mafunzo hayo kwa walimu ambao sasa watakwenda kufundisha watoto kwa namna rahisi itakayowawezesha kuelewa bila kutumia nguvu .


Ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili walimu wote wanaofundisha elimu ya awali waweze kufikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutoa elimu bora kwa watoto wadogo ambao wanaandaliwa kulitumikia Taifa hapo baadaye.Afisa Elimu Kata,Kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa Batlet Mfugale amesema ,watoto elimu ya awali wanahitaji kufundishwa kwa ukaribu zaidi ili waweze kujifunza na kujua kusoma kuandika na kuhesabu ili wawe wazuri zaidi wanapofika madarasa ya juu.


“Watoto wengi unakuta hawajui kusoma kuandika na kuhesabu wanapofika madarasa ya juu kwa sababu hawakuzingatiwa katika ufundishwaji kulingana na umri wao ,lakini kupitia mradi wa Watoto wetu tunu yetu kama ukizingatiwa,kusimamiwa na watoto wakapata stahili zinazotakiwa wataweza kumudu stadi zote tatu watakapokuwa madarasa ya juu kwa sababu elimu awali ndiyo msingi wa watoto wetu.”


Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano 2021/22-2025/26 inayolenga kuhakikisha mtoto anakua kwa utimilifu wake na hivyo Taifa kuwa na nguvu kazi yenye tija hapo baadaye.

No comments:

Post a Comment