Asila Twaha, MOROGORO
Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa ametoa wito kwa walimu wa elimu ya awali kushirikiana na viongozi wa Serikali, dini, walezi/wazazi kuwafuatilia watoto katika makuzi na malezi kwa kuwa ndio waliopewa dhamana ya kuwasimamia.
Dkt. Mtahabwa ameyasema hayo Juni 27, 2023 wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia alipokua akifungua Mafunzo ya Walimu wa Elimu ya Awali ya kuwezesha ujifunzaji wa Mtoto kulingana na hatua za makuzi ambapo mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi (BOOST).
“Jukumu kubwa la Wizara ya Elimu ni utoaji wa elimu nchini kwa kuandaa Sera, Sheria na Miongozo kunzia ngazi ya elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu na Ofisi ya Rais -TAMISEMI wanaolo jukumu la kusimamia utekelezaji wake ili kufikia malengo yaliyowekwa na kwa ubora” amesema Dkt. Mtahabwa
Amesema Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi ikiwa ni afua namba nne inayohusu upatikanaji wa maudhui na vifaa vya kujifunzia kwa watoto wa Elimu ya Awali kwa kuzingatia mahitaji ya watoto utekelezaji wa maudhui ya mtoto ni kufikia malengo na makuzi timilifu.
Dkt. Mtahabwa amesema, pamoja na utekelezaji wa maudhui ya mtoto lakini pia walimu hao watatakiwa kujifunza miongozo, vitabu, pamoja na vifaa mbalimbali ikiwemo miongozo ya utoaji wa elimu ya awali iliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu pamoja na mtaala na vifaa vyake kuchangamsha ujifunzaji shirikishi kwa mtoto wa darasa la awali.
Amewataka walimu kuwa karibu na watoto kwa kutoa huduma bora kwa kuzingatia mahitaji , kutoa matokeo yaliyo chanya sababu misingi wa mtoto huanzia katika ngazi ya elimu ya awali.
Kwa upande wa Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu(TSC) Bi. Paulina Nkwama amesema kupitia Mradi wa (BOOST) TSC katika eneo la shule salama imetoa kitabu cha Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu.
Ametoa rai kwa walimu hao kuisoma na kuijua miongozo na maadili ya utumishi wa walimu na kutimiza wajibu wao kwa kumlea mtoto kwa kuhakikisha anakua katika maadili ya kitanzania na kumuwezesha kitaaluma ili aweze kuwa mahiri na kuweza kuishi kulingana na watu walioelimika katika nchi yake na kulingana na mazingira.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Msingi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bw. Ally Swalehe amesema, mradi wa BOOST unajumla ya afua 8 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya shule.
Amesema, kwa mwaka 2022/23 Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa sh.bil.230 kuboresha elimu ya msingi na awali katika halmashuri zote 184 ambapo shule mpya 302 zinajengwa pamoja zikiwa na vyumba vya madarasa ya mfano kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali.
Vilevile, ameeleza kuwa, vyumba vingine vya madarasa vya mfano vya Elimu ya Awali 368 vinajengwa kwenye shule za msingi zilizopo kuptia mradi wa BOOST.
Pia, amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo walimu wa shule hizo zilizojengwa na kuziwekea vifaa vilivyoboreshwa vya Elimu ya awali kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya awali kujifunza kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment