Wananchi Wapongeza "Madaktari wa Mama" na Huduma za Mama na Mtoto Kituo cha Afya Ujiji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 8, 2023

Wananchi Wapongeza "Madaktari wa Mama" na Huduma za Mama na Mtoto Kituo cha Afya Ujiji


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

 
Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma wanaopata huduma za matibabu katika Kituo cha Afya Ujiji, wamekipongeza kituo hicho kwa kutoa huduma nzuri hasa za afya ya mama na mtoto.

 

Pongezi hizo zimetolewa leo katika halmashauri hiyo wakati timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Afya ilipotembelea kituo hicho kuona maendeleo ya mafunzo ya kuwajengea uwezo na utoaji huduma kwa mama na mtoto yanayotolewa na timu ya Madaktari Bingwa kwa watoa huduma wa afya wa kituo hicho ikiwa ni utekelezaji wa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Tanzania inaondokana na vifo vya mama na mtoto.

 


Ndoto hiyo ya Rais Samia inatekelezwa na Wizara ya Afya chini ya kampeni ijulikanayo kama "Madaktari wa Mama Samia" ambapo timu za Madaktari Bingwa kutoka hospitali mbalimbali nchini zimepelekwa katika baadhi ya Vituo vya Afya kuwaongezea ujuzi watumishi wa afya wa vituo hivyo juu ya utoaji huduma bora na sahihi za mama na mtoto.

 
Kwa upande wake Chausiku Shabani ambaye ni Mkazi wa Ujiji amesema kuwa, huduma za mama na mtoto katika Kituo hicho cha Afya ni nzuri na kutoa ushauri kwa Serikali kuendelea kuleta vifaa na kuwaongezea ujuzi zaidi watumishi wa kituo hicho ili kuimarisha huduma za afya.

 

Aidha, amemuomba Rais, Dkt. Samia kuongeza watumishi wa afya ili kurahisisha huduma zinazotolewa kituoni hapo.

 

"Huduma ni nzuri na tunahudumiwa vizuri, tunamshukuru Rais, Dkt. Samia kwa maono yake ya kuwaleta madaktari bingwa kwa ajili ya kutoa ujuzi wa kitabibu kwa watumishi wa kituo hiki kwani itawasaidia wananchi kupata huduma bora za afya ya mama na mtoto, pia nampongeza kwa kutukumbuka wanawake wenzie kwenye masuala ya uzazi", alisema Chausiku.

 

Naye Bi. Asia Kwaya amekipongeza kituo hicho kwa kazi nzuri ya kuhudumia wananchi ambapo amefafanua kuwa kazi nzuri inatokana na uwepo wa Madaktari na Wauguzi waliofanya kazi hizo kwa muda mrefu kituoni hapo ambao wanafahamu zaidi jinsi ya kutoa huduma za uzazi kwa kufuata maadili na miiko ya taaluma.


Vile vile, ameiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo na kuwakumbusha watumishi wa afya hasa ambao ni vijana kupunguza matumizi ya simu wanapokuwa ofisini kwani hali hiyo inapunguza ufanisi wa huduma hasa kwa wajawazito waliopo kwenye hatua za kujifungua.

 

"Kituo cha Afya Ujiji ni mbali na kituo kidogo kipo mwishoni kabisa lakini kinatoa huduma bora za mama na mtoto, hivyo hata tukiwa wajawazito katika maeneo yetu tunayoishi tunakumbuka kurudi kuja kujifungulia nyumbani", alisema Bi. Asia.

 

Kijana Msafiri Sindano ambaye ameongozana na mwenzi wake kwenye kliniki ya afya ya mama na mtoto inayotolewa katika kituo hicho, amekipongeza kituo hicho kwa kutoa mafunzo yanayowasaidia kufahamu lishe ya mama mjamzito, dalili za hatari na maandalizi ya kujifungua kwa wajawazito.

 

"Tunawashukuru watumishi wa kituo hiki kwa kutushawishi hata sisi wanaume kufika katika kituo na kupewa elimu ya malezi ya mama mjamzito na malezi ya mtoto mchanga, hii inaturahisishia kufahamu mapema kama kuna changamoto na kuwahi kumuona Daktari. Huyu ninayetarajia kumpata ni mtoto wa pili, kiufupi tangu nianze kupata huduma katika kituo hiki sijawahi kupata changamoto yoyote", alisema Msafiri.


No comments:

Post a Comment