MIRADI SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA IKAMILIKE KWA WAKATI- DKT.MATARAGIO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 14, 2026

MIRADI SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA IKAMILIKE KWA WAKATI- DKT.MATARAGIO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, ameitaka Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha kuwa miradi ya mafuta na gesi asilia inayoendelea nchini inatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili iweze kuendelea kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Dkt. Mataragio ametoa maelekezo hayo leo wakati alipokutana na menejimenti ya TPDC kwa lengo la kujadili fursa zilizopo katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia, changamoto pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta.

Aidha, Dkt. Mataragio ameiagiza TPDC, kuongeza vitalu vipya vya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.

“Ni muhimu TPDC ikaendelea kupanua maeneo ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kama mnavyofahamu rasilimali hii ni muhimu katika kutoa uhakika wa nishati nchini mfano kwenye uzalishaji wa umeme na kukuza uchumi wa viwanda." Amesisitiza Dkt.Mataragio

Kwa upande wake, Kamishna wa Petroli, Goodluck Shirima, amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia ili kuongeza matumizi yake katika sekta mbalimbali ikiwemo majumbani, viwandani na katika uzalishaji wa umeme.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutenga na kuandaa maeneo kwa ajili ya ushiriki wa sekta binafsi kwenye miradi ya usambazaji wa gesi, akibainisha kuwa miradi hiyo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati (flagship projects) inayolenga kuongeza matumizi ya gesi asilia.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema Shirika hilo litaendelea kutekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi wa Wizara kwa lengo la kuzidi kuiimarisha sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

“TPDC itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Nishati ili kuhakikisha miradi ya gesi asilia na mafuta inatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya Watanzania wote." Amesema Makame

Ziara ya Dkt. Mataragio TPDC ni muendelezo wa ziara zake katika Taasisi zinazosimamia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ikiwa ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Nishati kuimarisha usimamizi wa taasisi zake ili ziendelee kutekeleza majukumu kwa ufanisi lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo nchini.


No comments:

Post a Comment