YALIYOSEMWA NA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO DKT. MWIGULU NCHEMBA AKIWASILISHA HALI YA UCHUMI WA TAIFA MWAKA 2022 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA MWAKA 2023/24 UPANDE WA SEKTA YA AFYA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 15, 2023

YALIYOSEMWA NA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO DKT. MWIGULU NCHEMBA AKIWASILISHA HALI YA UCHUMI WA TAIFA MWAKA 2022 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA MWAKA 2023/24 UPANDE WA SEKTA YA AFYA.


✳️ A. HALI YA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI KWA MWAKA 2022/23👇🏾

❇️ Serikali imeendelea kuboresha huduma za kibingwa nchini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake ambapo jumla ya wagonjwa 25 wamepatiwa huduma ya upandikizaji wa uroto katika hospitali za Muhimbili na Benjamin Mkapa. Upatikanaji wa huduma hii hapa nchini umepunguza gharama za kupata huduma nje ya nchi kutoka shilingi milioni 250 hadi kufikia milioni 70 sawa na punguzo la asilimia 72 ya gharama zilizohitajika;

❇️ Kuanza kutoa huduma za kibingwa ya kibobezi ya kupunguza uzito kwa kuweka puto (Intragastric ballon) katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila ambapo jumla ya wagonjwa 87 wamepatiwa huduma hiyo; na kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha upandikizaji viungo na ukarabati wa wodi za watoto mahututi (NICU) katika hospitali ya Muhimbili – Mloganzila.

❇️ Kwa upande wa Hospitali za Rufaa za Kanda mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa majengo ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Bugando; kuendelea na ujenzi wa jengo la huduma za tiba - mionzi kwa magonjwa ya saratani katika hospitali ya KCMC; na kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU), jengo la huduma za dharura (EMD), chumba cha tiba mtandao, katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

❇️ Kwa upande wa Hospitali za Rufaa za Mikoa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya OPD, afya ya uzazi, EMD, ICU, upasuaji, mifupa, wodi, sehemu ya kufulia, damu salama na kichomea taka katika hospitali ya Njombe; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (asilimia 94) katika hospitali ya Simiyu; na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la afya ya uzazi na kuendelea na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi katika hospitali ya Geita ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98.


❇️ Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kufikia ngazi za chini ambapo inaendelea na: ujenzi wa hospitali 59 na ukarabati wa hospitali kongwe 19 za Halmashauri; ukamilishaji wa zahanati 300 katika halmashauri 184; na ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya 150, zahanati 300, na hospitali za Halmashauri 71.

❇️ Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za bima za afya, idadi ya watanzania wanaopata huduma za bima ya afya imeongezeka kutoka asilimia 21.2 mwaka 2019/20 hadi asilimia 30.6 mwaka 2021/22.

✳️ B. *MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA MWAKA 2023/24 KWENYE UPANDE WA SEKTA YA AFYA*👇🏾

❇️ Kuchochea Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa imelenga kuboresha maisha ya watu pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii. Miradi hiyo ni pamoja na: miradi ya afya kwa kuimarisha huduma za afya katika hospitali za kitaifa, hospitali za rufaa za kanda na mikoa; hospitali za halmashauri; vituo vya afya na zahanati; kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi;

❇️ Kuendeleza Rasilimali Watu: Kuendelea na utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali ya kukuza ujuzi nchini ili kuongeza ajira kwa vijana kwa kutoa mafunzo ya ufundi na stadi za kazi kupitia programu mbalimbali.

*MAJUMUISHO*👇🏾

❇️ Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji ili kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi, kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo ya watu, kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi zikiwemo huduma za afya, elimu, umeme na maji safi na salama mijini na vijijini pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa ajili ya masoko ya kimataifa hususan ya nchi jirani.

❇️ Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na athari za majanga mbalimbali ya asili na yasiyo ya asili yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, magonjwa na vita. Aidha, tutaendelea kuimarisha utekelezaji kwa kuweka mipango madhubuti ya kupunguza athari zitokanazo na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine ikiwemo kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa mbalimbali na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kukabiliana na Athari za UVIKO– 19. 

Imeandaliwa na Kitengo Cha Mawasiliano
*Wizara ya Afya* 🇹🇿
#TunaboreshaAfya #MtuniAfya #JaliAfyaYako ✅

No comments:

Post a Comment