Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe madarasa 51, Vyoo 63 na nyumba 1 ya waalimu ikiwa ni sawa na shule 7 zilizokamilika katika Wilaya ya Bahi.
Akipokea shule na miundombinu yake Senyamule amepongeza uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kukamilisha mradi huo tarehe 28 Juni 2023 ikiwa ni siku mbili kabla ya tarehe iliyopangwa na Mkoa yaani tarehe 30 Juni 2023.
“Bahi mnajipambanua sana katika suala la elimu, awali tu tulikuwa tunaziambia Halmashauri zingine zije zijifunze kwenu kuhusu kufaulu, leo tutawatuma kujifunza kuhusu mnavyojipanga kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati na viwango vya hali ya juu” Senyamule amesisitiza.
Amesema Mkoa wa Dodoma umepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya 16 zenye miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na michezo ya watoto na uzio kwa ajili ya madarasa ya awali.
Akikabidhi madarasa hayo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe amesema Wilaya yake imekamilisha ujenzi huo wa Shule na madarasa kwa muda ulioelekezwa kwa ubora na viwango elekezi, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa ya kufanikisha ujenzi huo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa naomba upokee Shule hii na madarasa ambayo yamekamilika kwa viwango vya ubora wa hali ya juu kwa niaba ya wana Bahi naomba utufikishie shukrani zetu kwa Mhe Rais” Amefafanua Mhe. Gondwe
Kwa upande wake Afisa Elimu Wilaya ya Bahi Mwl. Boniphace Wilson amesema kukamilika kwa madarasa hayo ni suluhu ya msongamano wa wanafunzi katika madarasa ya awali ambapo Wilaya hiyo ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya mbili zenye jumla ya vyumba 28, madarasa manne ya awali, majengo mawili ya utawala na vichomea taka.
Wilaya ya Bahi imekuwa Wilaya ya kwanza katika Mkoa wa Dodoma kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Boost ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa shule mpya za msingi, vyumba vya madarasa, madarasa ya mfano ya elimu ya awali, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.
No comments:
Post a Comment