Na Mwandishi wetu
Ujumbe wa biashara wa Misri unaojumuisha kampuni kubwa 15 umetembelea Tanzania kutafuta fursa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utalii na hoteli na kuanzisha ushirikiano na wafanyabiashara wa ndani.
Ujumbe huo uliowasili mapema wiki hii umekutana na kufanya mikutano na viongozi, kampuni za ndani na wadau wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa mkutano uliokutanisha kampuni hizo na yale ya nchini Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), Dk. Nkundwe Mwasaga amesema ujumbe huo unajumuisha kampuni kadhaa zinazofanya kazi katika fani ya Tehama, samani na vifaa vya hoteli.
Amesema kuwa serikali imeboresha sera na sheria pamoja na kanuni za uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Dk Mwasaga ameongeza kuwa nchi imekuwa ikifanya jitihada za kutekeleza zaidi mipango na mifumo kielektroniki na kukuza matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika huduma za umma.
“Kwa sasa tunawekeza nguvu zetu nyingi ili kuhakikisha kwamba tunatoa msaada wote unaohitajika kwa wabunifu wachanga ambao wameona fursa katika teknolojia zinazoibuka ili kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali kama vile usafirishaji, hoteli an huduma na maeneo mengine,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ujumbe umepata nafasi ya kutosha ya kukaa na kujadiliana na kampuni mbalimbali za teknolojia ya Tanzania na waanzilishi na itasaidia kujenga mahusiano imara ambayo yatakuza sekta ya TEHAMA kwa maendeleo endelevu.
Ofisa Mkuu wa operesheni wa Brightskies ya nchini Misri, Hicham Arafa, amesema Jumuiya ya Wasafirishaji nje ya Misri (Expolink) imekuwa na mafanikio chini ya udhamini wa Benki ya Kitaifa ya Misri na kwa ushirikiano na wakala wa uwakilishi wa kibiashara wa Misri na mabaraza yanayolengwa ya usafirishaji.
Amekiri kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na fursa nyingi za maliasili na uwekezaji na kutokana na jitihada za mamlaka za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kampuni hizo zinaona ni bora kuja kutengeneza mahusiano ya kibiashara na kampuni za Tanzania pamoja na serikali.
Amebainisha kuwa sekta ya TEHAMA ya Misri imekuwa ikikua kwa kiasi kikubwa ikitoa fursa pana kwa wawekezaji katika kutoa huduma nje, utafiti wa uhandisi na maendeleo (ER&D) na vifaa vya elektroniki.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga amesema kampuni hiyo itaisaidia Tanzania kuanzisha mifumo ya kidijitali ili kuisaidia nchi kuweza kukusanya vizuri mapato yote ya watalii.
“Tunajaribu kuzungumza na wenzetu kutoka Misri, tujifunze kutoka kwao jinsi wanavyosimamia utalii na mapato yao, tunajifunza jinsi wanavyokusanya mapato kutoka sekta hii muhimu kwa kutumia mifumo ya kidijitali,” amesema.
No comments:
Post a Comment