Wananchi wa Wilaya ya Songwe wametambulishwa uwepo wa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya Rare Earth Elements yanayotumika katika teknolojia ya kisasa ambayo yataisaidia dunia kupunguza changamoto ya athari za hewa ya ukaa (hewa sumu) kwa kutumia teknolojia safi itokanayo na madini hayo na kuepuka athari za mazingira kwa watu na mimea.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Kiruswa katika hafla ya kutambulisha rasmi kwa wananchi Leseni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Rare Earth Elements iliyofanyika katika Kijiji cha Ngwala wilayani Songwe.
Amesema Madini ya Rare Earth Elements ni miongoni mwa madini muhimu na ya kimkakati yanayohitajika sana duniani hususan katika matumizi ya maendeleo ya teknolojia ikiwemo utengenezaji wa betri za magari ya umeme, vifaa vya Simu, mota na teknolojia za kisasa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema uwekezaji katika Mradi wa Ngualla unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 486 na utazalisha ajira rasmi 800, ajira zisizo rasmi 3,000 katika kipindi cha ujenzi wa mradi ambapo baada ya kukamilika kwa mradi utazalisha ajira rasmi 250 na ajira zisizo rasmi 1,000.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kufanya ziara katika mkoa huo na kumuomba kushughulikia kero na changamoto zilizopo katika sekta hiyo mkoani humo ikiwemo miundombinu ya barabara pamoja na ukosefu wa nishati ya umeme.
"Mradi wa Ngualla ulisainiwa tarehe 17, Aprili, 2023 Ikulu jijini Dodoma na tunaamini Mradi ukianza uzalishaji asilimia kubwa ya vijana wetu watapata ajira na mapato ya mkoa wa Songwe yataongezeka," amesema Itunda.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Songwe Philipo Mulugo amesema Kampuni ya Peak Rare Earth Elements ina mahusiano mazuri na jamii inayozunguka eneo la mgodi ambapo mpaka sasa kampuni hiyo haijaanza uzalishaji lakini tayari imejenga shule, Kituo cha Afya, barabara na imepanga kujenga Kituo cha Polisi na nyumba ya Mkuu wa Kituo katika Kijiji cha Ngwala.
Naye, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Peak Rare Earth Elements Ismail Diwani amesema Kampuni ya Peak Resources ilianza utafiti wa Phosphate katika eneo hilo mwaka 2008 ambapo mwaka 2010 iligundua uwepo wa tani 890,000 za madini ya Rare Earth Elements yenye kiwango bora duniani na kupelekea kuachana na utafiti wa awali ili kuanza tafiti za Madini ya Rare Earth Elements na kukamilisha mwaka 2017.
Diwani amesema mwaka 2018 Kampuni hiyo iliamua kubadilisha jina kuwa Peak Rare Earth Elements ambapo kwa sasa kampuni hiyo inamilikiwa kwa ubia kupitia Kampuni ya Mamba kati ya Serikali kwa asilimia 16 na Peak Rare Earth Elements kwa asilimia 84.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe ambapo alipewa taarifa ya maendeleo ya shughuli za madini katika mkoa huo na kumpongeza Mkuu wa Mkoa huo kwa kusimamia vyema shughuli za sekta hiyo mkoani hapo.
No comments:
Post a Comment