Na Mwandishi Wetu,MBEYA
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) limeanzisha mfumo wa kielektroniki wa usajili wa miradi ili kuwarahisishia wawekezaji kufanyiwa tathmini ya athari ya mazingira(TAM).
Kutokana na hatua hiyo, limewataka wawekezaji wa miradi kutekeleza sheria ya mazingira inayotaka miradi kupata cheti cha TAM kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Ofisa Elimu ya Jamii wa NEMC, Suzan Chawe akizungumza kwenye banda la Baraza hilo katika maonesho ya nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini hapa, alisema baraza limerahisisha mchakato wa TAM kwa kuanzisha usajili wa miradi
kwa mfumo wa kielektroniki na kusogeza huduma katika ofisi za Kanda zinazopatikana nchini.
"Tunawakaribisha wenye sifa za kuwa washauri elekezi wa Mazingira kujisajili na kupata cheti cha utendaji kwa ajili ya kufanya TAM na ukaguzi wa mazingira,"alisema.
Meneja wa NEMC Kanda ya nyanda za juu kusini, Josia Mlunya, alisema katika banda hilo shughuli zinazofanyika ni kusajili wataalamu elekezi wa mazingira, usajili wa miradi kwa ajili ya cheti cha TAM.
"Pia tunatoa elimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, pamoja na kupokea malalamiko na maoni yanayohusu mazingira na kuyashughulikia,"alisema.
No comments:
Post a Comment