Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekipongeza Kituo cha STEM Inspire kilichopo mkoani Tanga kwa kutumia Teknolojia na vitu vinavyopatikana ndani ya nchi katika kuendeleza masomo ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu.
Akizungumza baada ya kutembelea kituo hicho kuona shughuli mbalimbali zinazofanyika Prof. Mkenda amesema kuwa amepata fursa ya kuangalia na kujifunza kuhusu mbinu zinazotumiwa na wataalam hao kumsaidia mjifunzaji kupata uelewa namna Sayansi inavyofanyakazi katika Karne hii.
"Hapa nimeona vitu vizuri, kama ambavyo mmeviona, waliniomba nije nitazame nione wanachokifanya na wanataka tusaini hati ya makubaliano na wizara yetu kwa ajili ya ushirikiano.
"Sasa nimeona wanavyofundisha Sayansi kwa kutumia Teknolojia na vitu vinavyopatikana Tanzania, lakini hapa mafunzo yanafanyika kwa vitendo zaidi na huko tunakoenda mbeleni ni muhimu kuzingatia mfumo shirikishi wa ufundishaji wa watoto wetu ili waweze kufikiri na kufanya uvumbuzi wenyewe". alisema Prof. Mkenda
Ameongeza kuwa, serikali itashirikiana na Kituo hicho ili kuanzisha kituo kingine kikubwa zaidi mkoani Dodoma, kuwapatia nafasi Wakuu wa mikoa, Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri kutembelea kwa ukaribu kujionea manufaa yake na hatimaye kuongeza msukumo wa ujenzi wa Vituo hivyo nchi nzima.
"Najua haitawafikia Wanafunzi wote, lakini itaanza kuhamasisha, na mbele ya safari kwenye Mitaala mipya itabidi ishuke kwenye Kata, na hatimaye kila shule, kwa sababu vitu karibu vyote vinapatikana kirahisi ndani ya nchi". Alieleza Prof. Mkenda
Akieleza kuhusu kazi ya kituo hicho Mwanzilishi mwenza wa Mradi wa STEM Park Inspire Bw. Lwidiko Edward amesema ni kuhakikisha inalea Watoto kutokana na udadisi wa kiasili wa Sayansi mpaka kuwatengeneza kuwa Wanasayansi halisi kwa kutumia mbinu
mbalimbali.
Pia ameongeza kuwa kituo kinaandaa mazingira kwa ajili ya kuwapatia hamasa Watoto kusoma, na ndio ya dhana ya kujenga Vituo hivyo jijini Dar es Salaam na Tanga pamoja na kuhakikisha watoto wanapata kujifunza ujuzi na fursa za kuendelea na masomo ngazi za juu.
"Kwa sababu nchi zote zilizoendelea karibu asilimia 60 mpaka 70 ya mapato yao ya ndani ya nchi yanatokana na taaluma za Sayansi, Uhandisi, Teknolojia na hesabu. na Tanzania ili tufike huko, tunahitaji wanataaluma wengi katika maeneo hayo, kwa hiyo ndio maana tumekuwa tukifanya hivi karibu miaka minane sasa". amefafanua Bw. Lwidiko
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dr. Amos Nungu amesema wanajivunia Mradi huko unaosaidia kujenga Umahiri na kuweka mazingira rafiki kwa wototo kujifunza kwa ari kubwa.
Vile vile amebainisha kwamba, Mradi huo umeleta mafanikio ikiwemo baadhi ya Wanafunzi kushiriki na kufanya vizuri katika Mashindano ya Kimataifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na wengine kufadhiliwa kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo.
No comments:
Post a Comment