
Na Mwandishi Wetu - Arusha
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa barabara ya Esso–Longdong yenye urefu wa kilomita 1.8 kwa kiwango cha lami katika Jiji la Arusha.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TARURA, Meneja wa TARURA Wilaya ya Arusha, Mhandisi Godfrey Bwire amesema barabara hiyo imekamilika na kazi iliyobaki ni uwekaji wa taa za barabarani.
“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali kupitia TARURA imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Eso–Longdong kwa kiwango cha lami. Kilichobaki ni uwekaji wa taa za barabarani ambapo mara baada ya kukamilika wananchi wataweza kufanya biashara zao nyakati za usiku na usalama unakuwepo kwa wafanyabiashara” alisema.
Amesema barabara hiyo imejengwa kwa kutumia mapato ya ndani na ina umuhimu mkubwa katika kupunguza msongamano wa magari hasa katika eneo la soko la Kilombero linalojengwa kupitia mradi wa TACTIC.
Amefafanua kuwa barabara hiyo itatumika kama njia mbadala kwa watumiaji wa barabara wanaotoka Mromboo badala ya kuzunguka eneo la Sombetini, hivyo kusaidia kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano.
Aidha, amesema utekelezaji wa miradi ya TACTIC unaendelea katika mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo jumla ya shilingi bilioni 20.7 zinatumika kuboresha barabara kilomita 10.2 kwa kiwango cha lami na Shilingi bilioni 30.6 zitatumika kujenga Soko la Kilombelo, Soko la Kwamorombo, Standi ya Mabasi na Bustani ya Themi.
Amezitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na barabara ya Engosheratoni yenye urefu wa kilomita 4.8, barabara ya Olasiti kilomita 3.96 na barabara ya Oljoro yenye urefu wa kilomita 1.475 ambako kunajengwa kituo kikubwa cha mabasi Jijini Arusha.
Amesema miradi hiyo inalenga kuboresha usafiri na kuleta karibu huduma za jamii, kupunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Jiji hilo.
Mbali na miradi hiyo, amesema kuna miradi mingine inayotekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund), ikiwemo ujenzi wa barabara kutoka Kijenge Juu-Ngulelo Km 0.35, Boma Siara Km 0.475, Oljoro-Kisimani Km 0.4, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza msongamano wa magari na kuboresha barabara katika Jiji la Arusha.
Aidha, amesema mipango inaendelea ya kujenga barabara nyingine kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara ya Kibo yenye urefu wa Km 3.55 kutoka Safina hadi Arusha Girls kupitia barabara ya Uwanja wa Ndege, pamoja na barabara ya Lemala (TBL-Tanesco) yenye urefu wa kilomita 4.17.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi, Mhandisi Bwire amesema wamepokea kwa furaha ujenzi wa barabara hizo kwani hapo awali zilikuwa na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua na vumbi wakati wa kiangazi.
Amewataka wananchi kutunza miundombinu hiyo kwa kuepuka kutupa taka katika mitaro ya maji na kuhakikisha inasafishwa mara kwa mara ili kuruhusu maji kupita vizuri.
Pia amewahimiza kulinda taa za barabarani ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia kuimarisha usalama wakati wa usiku.
Amesema serikali hutumia gharama kubwa kujenga miundombinu hiyo hivyo ni wajibu wa wananchi kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya wote.

No comments:
Post a Comment