* Wamo pia Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu kutoka nchi mbalimbali
* Rais Samia ashangiliwa kwa kuhutubia wageni wa nje kwa Kiswahili
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan ameendelea kuipaisha Tanzania kimataifa baada ya kufanikisha ujio jijini Dar es Salaam wa marais wasiopungua sita na Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu kadhaa kutoka nchi mbalimbali duniani.
Viongozi hao waliwasili Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu (Africa Heads of State Human Capital Summit) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, leo tarehe 26 Julai, 2023.
Marais waliowasili Dar es Salaam ni pamoja na Rais William Ruto wa Kenya, Rais Andry Rajoelina wa Madagascar na Rais Carlos Vila Nova wa São Tomé na Principe.
Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Wonie Bio, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, pia ni miongoni mwa marais waliokuja Tanzania.
Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na wageni wengine mashuhuri kutoka Uganda, Rwanda, Sudani Kusini, Namibia na nchi nyingine nao wamekuja Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo.
Akiwa ni mwenyeji wa marais hao, Rais Samia pia alifanya mazungumzo ya pembeni na baadhi ya viongozi ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na mataifa ya nje.
Rais Samia aliwakosha wajumbe wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kwingine duniani baada ya kuamua kuhutubia kwa kutumia lugha ya Kiswahili, kitendo kilichofanya ashangiliwe na wahudhuriaji wa mkutano huo.
Katika hotuba yake, ambayo ilitafsiriwa kwa wageni wasiojua Kiswahili, Rais Samia alihimiza uwekezaji katika sekta za elimu na afya ili kuweka msingi mzuri kwa watoto kukua vizuri kiakili.
"Tunapozungumzia uwekezaji katika rasilimali watu, ni kuhakikisha kuwa uwekezaji unaanza tangu mtoto anapozaliwa. Kwa maana ya upatikanaji wa lishe bora na chanjo stahiki, ili kuondoa udumavu ambao mara nyingi hupunguza kiwango cha uelewa na uwezo wa kusoma vizuri kwa watoto hao," alisema.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuwekeza kwenye rasilimali watu kama chachu ya maendeleo endelevu.
"Hatuwezi kulikomboa bara letu kiuchumi kama hatutoelekeza nguvu zetu kwenye maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwapa wananchi maarifa na ujuzi unaohitajika katika kuyatumia na kuyabadilisha mazingira yao kwa manufaa yao," aliongeza.
Samia alisema kuwa ni muhimu kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha kuwa wanaangalia, wanatathmini na kusimamia mageuzi yote muhimu ili kuliwezesha bara hili litumie uwezo na rasilimali zake kujikomboa kiuchumi.
Rais aliwakumbusha viongozi wenzake kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wa Afrika ni vijana chini ya umri wa miaka 25, ambao amewataja kuwa ni rasilimali kubwa ya maendeleo.
"Afrika ndilo bara lenye vijana wengi zaidi, na takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2050, Afrika itatoa nchi 10 zenye idadi kubwa ya vijana duniani kwa mujibu wa taasisi ya World Economic Forum na ikikadiriwa kuwa ikifika mwaka 2030, Afrika itakuwa na 42% ya vijana wote duniani."
No comments:
Post a Comment