Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Kamati ya kitaifa ya kupambana na biashara haramu ya binadamu kwa kushirikiana na wadau wengine imetakiwa kuongeze jitihada za utoaji elimu kwa umma ili kukomesha biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
Hayo yamebainishwa leo July 30,2023 Jijini Dodoma katika taarifa iliyosomwa na afisa uchunguzi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Pontian Kitorobombo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume wa Jaji mstaafu Mathew Mwaimu katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu duniani .
Kitorobombo amesema serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inatekeleza Mpango Kazi wa miaka mitatu wenye dira ya kuifanya nchi iondokane na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na kutoa huduma bora kwa wahanga wa biashara hiyo.
“usafirishaji haramu wa binadamu ni janga linaloendelea kukua na kuathiri ustawi wa wananchi hususani wanawake, vijana na watoto ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na tatizo hili,”amesema.
Aidha ameongeza kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 zinaainisha kuwa binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa hivyo, kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru na kufanya kazi pamoja na kupata ujira unaolingana na kazi yake.
Amesema pamoja na jitihada hizo THBUB imebaini kuwa bado wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya usafirishaji haramu na utayari wa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanapotishiwa au kulazimishwa kutoa watoto wao.
Akizungumza kwa niaba ya Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma Padri Filo Nguruwe amesema mwanadamu yeyote anayeuzwa katika biashara hiyo haramu anakosewa utu wake, hawezi kujumuika na Mwenyezi Mungu maisha yake yote bali maisha atakuwa anamlalamikia na hawezi kujitawala atakuwa anatawaliwa.
“Mwenyezi Mungu ametupa vipaji ili tuweze kufahamiana, ili tuweze kufahidi kalama mbalimbali ambazo Mungu ametupa lakini baadhi ya wanadamu wanegeuza vitu hivyo kuwa sehemu ya kuwauza wenzao hili halimpendezi Mwenyezi Mungu,”amesema.
Ameongeza kuwa mambo yanayofanywa na wanadamu wengine yanaweza kuwa dhambi ya yule anayefanya tendo hilo lakini pia inakuwa dhambi ya jamii kwa wale ambao wameliona tukio na wakakaa kimya.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Godwin Gondwe amesema ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha inatoa ripoti kwa mamlaka husika endapo wataona kundi la watu wamekusanywa sehemu moja hawaeleweki wapi wanakwenda.
Ikumbukwe kuwa kila mwaka ifikapo July 30 ulimwengu huadhimisha siku ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu duniani ambapo ilipitishwa na naraza kuu la Umoja wa Mataifa Novemba 15, 2000 kupitia Azimio Na. 55/25, na ilianza kuadhimishwa rasmi Julai 30, 2003.
Lengo la maadhimisho hayo ni kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ukatili, udhalilishaji na unyonyaji unaotokana na biashara hiyo.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “Tuwafikie wahanga wote wa usafirishaji haramu wa binadamu yeyote asiachwe nyuma” ikiwa inasisitiza kuimarisha jitihada za kutoa elimu kwa wananchi, kusaidia wahanga na kuendeleza mapambano ili kutokomeza biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini.
No comments:
Post a Comment