Na. WAF - Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kupunguza uagizaji wa bidhaa za Afya ikiwemo dawa kutoka zaidi ya asilimia 80 hadi chini ya asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Julai 21, 2023 kwenye hafla fupi iliyofanyika Hotel ya Johari Rotana na kuwakutanisha wadau pamoja na wawekezaji mbalimbali ambao ni wasambazaji wa bidhaa za Afya.
“Katika mazungumzo yenu tunatumai mtaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha tunapunguza uagizaji wa bidhaa za Afya kutoka zaidi ya 80% hadi chini ya 50% ifikapo 2030”, amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Afya ikiwemo kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za Afya nchini Tanzania ikiwemo Dawa.
“Tunaendelea kuimarisha viwanda vyetu lakini pia Soko tunalo na tunaungana na nchi nyingine nyingi kupitia kanda za EAC na SADC ili upatikanaji wa huduma bora za Afya uwe rahisi na tuendelee kupata wawekezaji”, amesema Waziri Ummy
“Serikali kupitia Wizara ya Afya tunawakikishia wadau na wawekezaji wetu tutaendelea kusaidia katika uwekezaji wa huduma za Afya ikiwa ni pamoja na soko la bidhaa zitakazozalishwa”, amesema Waziri Ummy
Amesema, Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha na kuboresha mfumo wake wa Afya kupitia ahadi yake ya kugharamia huduma za Afya ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 600
Mwisho, Waziri Ummy amewataka wawekezaji hao kuendeleza mazungumzo katika mkutano huo wa "Chat and Dine" ili kuleta matokea mazuri ya wauzaji bidhaa, mawakala, wafanyabiashara wa bidhaa za Afya na wazalishaji wa ndani ili Serikali iendelee kuboresha huduma hizo.
No comments:
Post a Comment